Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Wednesday, September 24, 2014

Zifahamu dalili za shambulio la moyo




Dk Fadhili Emilly

Moja ya magonjwa hatari sana ambayo yanaweza kumpata mtu yeyote ni ugonjwa wa shambulizi la moyo. Ugonjwa huu upo katika orodha ya magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanaume na wanawake.

Kwa kawaida ugonjwa huu hutokea pale ambapo sehemu ya nyama ya moyo inapoharibika au kufa kutokana na kukosa damu ya kutosha.

Je tatizo hili husababishwa na nini?
Husababishwa na kuziba kwa mishipa ya damu inayosambaza damu katika moyo (coronary artery blockage) kutokana na mafuta mabaya mwilini (atherosclerotic plaque).
Watu gani wapo katika hatari ya tatizo hili?
Watu walio katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa huu ni pamoja na wale wenye umri mkubwa hususani kuanzia miaka 45 kwa wanaume na wanawake ni kuanzia miaka 55, wavutaji wa sigara, watu wenye mafuta ya lijamu katika damu au wale wenye mafuta mabaya aina ya triglycerides na low density lipoprotein kwa kiwango kikubwa katika damu zao.

Wengine walio katika hatari ni wale wenye kisukari, shinikizo la damu, walio na unene kupita kiasi (obesity), wenye matatizo sugu ya kushindwa kufanya kazi kwa figo zao (chronic renal failure), moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure).

Mbali na hao wengine ni wale wenye msongo wa mawazo, wanywaji wa pombe kupita kiasi, watumiaji wa madawa ya kulevya hasa ‘cocaine’ na ‘methamphetamine’ hali kadhalika na wale wenye upungufu wa vitamin B2, B6, B12 na folic acid.

Dalili za shambulizi la moyo
Dalili za tatizo hili ni maumivu makali ya ghafla kifuani ambayo husambaa kwenye taya, shingo, bega na mkono wa kushoto, kupumua kwa shida, kutoka jasho kwa wingi sana (diaphoresis), kuhisi mapigo ya moyo yanapiga haraka (palpitations), kichefuchefu na kutapika.

Sambamba na dalili hizo nyingine ni kupoteza fahamu na kuchoka haraka.

Shambulizi la moyo limehusishwa na nini?
Tafiti mbalimbali zimehusisha mambo yafuatayo na shambulizi la moyo
• Msongo wa mawazo
• Maambukizi hasa vichomi vinavyosababishwa na vimelea vya ‘chlamydophila pneumonia.’

Vipimo na uchunguzi
• ECG ni kipimo ambacho hutumika kuonesha ni sehemu gani ya moyo iliyoathirika
• Coronary angiography hiki husaidia kuangalia wapi ambapo mishipa ya damu imekuwa myembamba sana kupita kiasi (narrowing of vessels) au kuziba.
• Cardiac markers levels
• X-ray ya kifua (chest X-ray)
•Myocardial Perfusion Imaging (MPI), kipimo hiki hufanywa kwa kutumia mashine maalum ya PET Scan ambapo kinauwezo wa kugundua tatizo la shambulizi la moyo, huchunguza kikamilifu maumivu ya kifua, huangalia mwelekeo wa tiba ya kuzuia damu kuganda, hutoa mwelekeo wa ugonjwa wa shambulizi la moyo kama ni mzuri au mbaya, hutathimini ubora wa tiba ya shambulizi la moyo kabla na baada ya mgonjwa kupata tiba, huweza kutambua hata shambulizi la moyo ambalo si rahisi kugundulika kwa kutumia vipimo vingine na pia hutathimini ukubwa wa tatizo la shambulizi la moyo. Hata hivyo kwa sasa kipimo hiki hakipatikani nchini kwetu.

Ili kuweza kutambua uwepo wa tatizo hili, mwaka 1979, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliweka vigezo vya kutambua shambulizi la moyo. Vigezo hivyo ni pamoja na historia ya kuwa na maumivu ya kifua zaidi ya dakika 20, mabadiliko katika kipimo cha ECG, kupanda na kushuka kwa kipimo kiitwacho kitaalamu ‘cardiac biomarkers’

Matibabu
Shambulio la moyo ni tatizo linalohitaji matibabu ya dharua na lisipotibiwa kwa haraka husababisha kifo katika muda mfupi sana tangu mgonjwa apatwe na tatizo. Matibabu ya tatizo hili hujumuisha kumpa mgonjwa hewa ya oksijeni, mgonjwa hupewa vidonge vya Aspirini ndogo kuzuia damu kuganda (thrombolytic) kwa ajili ya kuyeyusha damu iliyoganda na hivyo kuzibua mirija midogo ya damu katika moyo iliyozibwa na kuganda huko kwa damu.

Vile vile mgonjwa hupewa dawa za kuweka chini ya ulimi kiitwacho ‘nitrogylycerin’ (glyceryl trinitrate) ambazo husaidia kutanua mishipa ya damu (vasodilatation), dawa mbalimbali za kutuliza maumivu kwa mfano morphine, dawa ya kuyeyusha mafuta katika mishipa ya damu kama vile ‘clopidogrel’ au upasuaji (CABG)

Njia za kuzuia shambulizi la moyo
• Kuacha kuvuta sigara
• Kufanya mazoezi mara kwa mara
• Kupunguza unywaji wa pombe
• Kubadilisha aina ya mlo. Kupunguza mafuta katika mlo na chumvi.
• Kutumia mafuta ya samaki (omega-3 fatty acids)

Aidha, kuna utafiti unaosema kuwa uchangiaji damu hupunguza hatari ya magonjwa ya moyo hasa kwa wanaume.

Madhara ya shambulizi la moyo
• Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure)
• Matatizo katika mfumo wa mapigo ya moyo (Atrial fibrillation) ambayo hatimaye hupelekea kifo.
• Shambulizi la moyo kurudia mara ya pili
• Kifo cha ghafla (sudden death)

Makala haya yameletwa kwenu na The Fadhaget Sanitarium Clinic, ambao hutoa huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa kutumia mimea asilia. Makao makuu yao ni Mbezi Beach Afrikana njia ya Salasala, Dar es Salaam. Au wasiliana nao kupitia 0712 705 158 / 0757 931 376
Hakikisha hupitwi na gazeti lako la TABIBU Alhamisi wiki hii kwa shilingi 500/= tu

No comments:

Post a Comment