SIMBA, YANGA KUONESHANA UBABE
DIRISHA DOGO
Na Mwandishi wetu
DIRISHA dogo la usajili kwa timu za Ligi Kuu
Bara na zile zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza litafunguliwa rasmi Novemba 15
wakati timu za Ligi Kuu zikiwa zimecheza mechi saba pekee tofauti na 13 kama
ilivyokuwa msimu uliopita.
Dirisha hilo litafunguliwa Desemba 15 ambapo
klabu za Yanga na Simba zinatarajiwa kuwa kati ya timu ambazo zitanufaika na
usajili huo kutokana na uhitaji mkubwa wa wachezaji wapya kwenye vikosi hivyo.
Simba itasajili kiungo mkabaji wa kusaidiana
na Jonas Mkude, mabeki wawili wa pembeni pamoja na straika mmoja ili kuimarisha
kikosi hicho ambacho hakijaonja ushindi wowote katika mechi nne za mwanzo msimu
huu.
Hata hivyo, dirisha la mwaka huu halitarajiwi
kuwa na usajili wa kihistoria kama ilivyotokea kwenye usajili wa dirisha dogo
msimu uliopita ambapo Yanga ilifanya usajili wa wachezaji wawili wa zamani wa
Simba, Emmanuel Okwi na kipa Juma Kaseja kwa fedha za maana.
Lakini wapo baadhi ya wachezaji ambao dirisha
dogo litakuwa na mkosi kwao.
Wachezaji ambao wanatarajia kufunguliwa milango ya
kutokea ni pamoja na Uhuru Seleman, Ivo Mapunda, Pierre Kwizera na Amri Kiemba
wa Simba wakati Said Bahanuzi na Hamis Thabiti wa Yanga nao wakiwa shakani.
Ismail Diara wa Azam naye huenda akakumbana na panga kwenye dirisha hilo.
Mbeya City nayo huenda ikafanya usajili wa
straika mpya kikosini hapo kutokana na safu yao ya ushambuliaji kushindwa
kufunga.
C. RONALDO: MAN U ITASHINDA LIGI KUU
UINGEREZA
London, England
Mchezaji nyota
wa klabu ya Real Madrid, Christiano Ronaldo amebashiri kwamba klabu ya
Manchester United maarufu kama ‘Mashetani Wekundu’ itashinda Ligi Kuu ya Uingereza chini ya
ukufunzi wa Louis Van Gaal.
Kulingana na gazeti la Mirror nchini
Uingereza, mchezaji huyo anaamini kwamba klabu hiyo aliyoichezea miaka ya 2003
hadi 2009 imefanikiwa kupata meneja mwenye uwezo wa kuiweka timu hiyo katika
kiwango ilichowekwa na aliyekuwa kocha wake Sir Alex Ferguson.
CR-7 kama anavyojulikana na wengi amesema
kuwa japokuwa klabu ya Chelsea chini ya ukufunzi wa Jose Mourinho itamaliza katika
nafasi ya kwanza msimu huu, kocha Van Gaal atafufua matumaini ya Manchester
United.
“Van Gaal ni kocha mzuri ambaye ataifanya
Manchester United kuwa bingwa tena na kama si mwaka huu basi mwaka mmoja kutoka
sasa,” alisema Ronaldo.
NAHODHA WA BAFANA BAFANA AUAWA
Johannesburg, Afrika
Kusini
Nahodha ambaye
pia ni golikipa wa timu ya soka ya Taifa la Afrika Kusini Senzo Meyiwa
amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana, jeshi la polisi
la nchi hiyo limesema.
Tukio hilo limeripotiwa kutokea katika nyumba
ya mpenzi wake iliyopo katika mji wa Vosloorus kusini mwa Johannesburg.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27
aliichezea klabu ya Orlando Pirates na alicheza mechi nne zilizopita za timu
yake ya taifa katika mechi za kufuzu za fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Jumamosi alikuwepo katika tukio la timu yake
pindi waliposonga mbele katika nusu fainali ya ligi ya Afrika Kusini.
Katika maelezo yake, jeshi la polisi la
Afrika Kusini limesema kwamba Meyiwa ameripotiwa kufariki wakati akiwasili
hospitalini.
UBAGUZI WA RANGI
WALITAFUNA SOKA
Na Juma Diwani
Mshambuliaji wa
timu ya Ghana anayeichezea Klabu ya Al Ains, Asamoah Gyan amemshtumu mchezaji
wa timu ya Al Hilal, Mihai Pintilii kwa kutoa matamshi ya ubaguzi wa rangi
wakati wa mechi ya raundi ya pili ya nusu fainali za Klabu Bingwa barani Asia
siku ya Jumanne.
Kisa hicho kilitokea baada ya Gyan kupewa
kadi nyekundu baada ya kumchezea visivyo Salem Al-Dawsari ikiwa zimesalia
dakika 20 kwa mechi hiyo kukamilika.
Pintilii ambaye ni raia wa Romania, alimkaribia
Gyan ili kutoa hasira zake hatua iliyosababisha mvutano kati ya wachezaji
kutoka pande zote mbili.
“Pintilii alinitolea matamshi machafu,” alisema
nahodha huyo wa timu ya Ghana.
Gyan aliongeza kuwa Pintilii hakuwa na haki
ya kutoa matamshi aliyoyatamka.
“Hana haki kuniambia yale aliyoniambia tena aliniambia
maneno yalionikasirisha na alichoniambia, unaweza kumuuliza.” alisema Gyan.
Gyan aliweka ujumbe wake katika mtandao wa Twitter
hivi karibuni akisema kuwa mchezaji huyo alimtolea matamshi ya ubaguzi.
Sanjari
na hilo, ni tukio la hivi karibuni la mshambuliaji wa Liverpool kutoka Italia Mario Balotelli aliyetukanwa
kutokana na rangi ya ngozi yake kupitia kwa mtandao wa kijamii wa Twitter.
SIMBA: MECHI 3, DROO 3,
POINTI 3, YANGA MAMBO POA
Na Kennedy Chaya, Dar
Klabu ya Simba ya Dar es
Salaam msimu huu wa ligi kuu ya Vodacom imeanza kwa kusuasua, jambo ambalo
halifurahishi mashabiki wake.
Timu hiyo ambayo imecheza mechi
tatu, imetoa sare tatu, hivyo kuwapa pointi 3 hali ambayo katika mechi zote iliyocheza
imeonesha soka la kawaida tofauti na mategemeo ya mashabiki wao.
Simba Jumamosi iliyopita
ilicheza na Shinyanga United, timu changa iliyopanda daraja msimu huu lakini Wekundu
hao walishindwa kufurukuta na hatimaye kulazimishwa sare na timu hiyo hali
ambayo mashabiki wengi wa Simba walisikika uwanjani hapo wakilalamika kutoridhika
na mwenendo wa timu yao.
Mashabiki hao walionekana kutofurahia
ushindi wa droo, na hivyo kuwaomba wachezaji wao kucheza kwa kujituma zaidi
uwanjani sambamba na kocha Phiri kuweka mfumo ambao utaiwezesha timu hiyo
kupata matokeo mazuri.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa
upande wa Simba, mahasimu wao timu ya Yanga ikionesha mambo yao kunyooka baada
ya kupata ushindi wa pili mfululizo ambapo Jumapili iliyopita iliiadhibu timu
ya Ruvu Shooting kwa jumla ya mabao 2-1.
Timu ya Yanga sasa imefikisha
pointi sita ikiwa nyuma ya bingwa mtetezi wa ligi hiyo Azam Fc.
Timu za Yanga na Simba msimu
huu zinahitaji jitihada zaidi katika kupata matokeo mazuri, kinyume chake
wategemee kupata matokeo mabaya kutokana na ligi hiyo mwaka huu kuonesha
ushindani wa hali ya juu.
No comments:
Post a Comment