Na Seif
Oddo
Tende ni tunda ambalo limethibitishwa kuwa na manufaa
makubwa katika mwili wa binadamu endapo litatumika ipasavyo.
Tunda hili ni maarufu katika nchi za mashariki ya kati na
sehemu nyingine duniani. Lakini asili ya tunda hili ni kutoka katika nchi za
kiarabu na liliingia Afrika Mashariki mnamo karne ya 7.
Nchini Tanzania tende hupatikata kwa wingi kisiwani Zanzibar
pamoja na Pemba, ambapo imekua kama ni sehemu ya chakula cha kiutamaduni
visiwani humo. Mbali na ladha yake nzuri ya tenda, lakini pia tunda hili
limekuwa likitajwa hasa katika vitabu vitukufu vya dini.
Aidha, tunda hili limekuwa likitumiwa sana na waumini wa
dini ya Kiislamu hususani katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Ambapo
Shekhe Khalfan Tiwany wa Chakechake Pemba anaeleza kuwa, tende ni miongoni mwa
vyakula vilivyotajwa katika Quraan Tukufu. Huku akiongeza kuwa, katika kisa
maarufu cha kuzaliwa Nabii Issa, mama yake Bi. Maryam aliamriwa kula tende
baada ya kujifungua, ili kurudisha damu nyingi aliyoipoteza baada ya kujifungua
pamoja na kurudisha nguvu ya mwili wake kwa haraka.
Mbali na hayo, wataalam wa tiba wamethibitisha kuwa tende ni
chanzo cha virutubisho na nishati mwilini, pia huwezesha kuupatia nguvu mwili
kwa haraka sana na hii ndio sababu ya tunda hili kutumika kwa wingi katika
Mfungo wa Ramadhani, kwani waumini waliofunga hulitumia tunda hili ili
kurudisha nguvu na nishati iliyopotea mchana kutwa walipokuwa wamefunga.
Wataalam wanaendelea kueleza kwamba, ndani ya tende kuna
virutubisho kama vile ‘calories,’ ‘calcium,’ ‘protein,’ ‘potassium,’ ‘magnessium,’ ‘phosphorous,’ ‘vitamin A’
‘foliate’ na ‘carbohydrates,’ ambavyo vyote ni muhimu katika miili yetu kiafya.
Hata hivyo, Dk, Ally Khamis wa Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja
Kisiwani Zanzibar ameeleza kuwa, tende ni chakula cha afya na huwa na
mkusanyiko wa ‘vitamin A,’ ambayo
husaidia katika kuongeza nuru ya macho, pia kuna madini ya ‘calcium,’ ambayo husaidia kuimarisha
mifupa, hali kadhalika ndani ya tunda kuna ‘vitamin
B6’ na B12, ambazo husaidia katika usagaji na ufyonzaji mzuri wa chakula na
kuingia katika mishipa ya damu.
Hali kadhalika, tunda hili linaelezwa kuwa na uwezo wa kutoa
kinga dhidi ya maradhi ya saratani ya tumbo (Colon Cancer). Pia huweza
kuimarisha moyo na kuukinga dhidi ya maradhi.
Mbali na hayo, tende pia hutibu maradhi ya tumbo kama vile
kujaa gesi, kuharisha na kuchafuka kwa tumbo. Pia wataalam wanaeleza kuwa tende
husaidia kuondoa sumu mwilini na kusaidia kuongeza nguvu za kiume endapo
litatumika kwa kufuata ushauri wa kitabibu.
Tende ni tunda pekee lenye uwezo wa kuupa mwili vitu vinne
kwa wakati mmoja ambavyo ni protini, wanga, vitamin na mafuta. Pia tende ni
tunda ambalo huyeyuka haraka sana tumboni, hivyo kutolipatia tumbo shida ya
kufanya umeng’enyaji (Digestion).
Sambamba na hayo, wataalam wa afya wanaeleza kuwa, tunda
hili husaidia kutanua misuli ya mji wa mimba na hivyo basi humsaidia mwanamke
kutopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua. Aidha, wataalam wa afya
wanaendelea kueleza kwamba tende ni chakula bora kwa wanawake wanaonyonyesha
kutokana na kusaidia kuyapa maziwa virutubisho muhimu ambavyo humfanya mtoto
kuwa na afya bora.
Mbali na hayo, tende ni chanzo kizuri cha madini ya chuma,
ambayo husaidia kuwapa ahueni watu wenye upungufu wa damu mwilini. Hivyo basi
mbali na kupenda kutumia tende kipindi cha Mwezi wa Ramadhani tu, ni vizuri
tukatumia siku zote kama tunavyotumia vyakula vingine, ili kuweza kuimarisha
afya zetu kikamilifu.
Makala kama hizi hupatika katika gazeti la TABIBU ambalo
linatoka kila siku ya Alhamis na kupatikana nchi nzima kwa shilingi 500/=
No comments:
Post a Comment