Ebola ni mojawapo ya virusi hatari zaidi ulimwenguni, lakini
ugonjwa huu hauambukizwi kupitia hewa, hivyo basi huwezi kuambukizwa ebola kama
homa ya kawaida.
Madaktari wanasema kuepuka Ebola ni
rahisi sana iwapo mtu atafuata tahadhari hizi muhimu zaidi:
1. Nawa mikono kwa sabuni na maji
Nawa mikono kila baada ya shughuli
yoyote, hakikisha unatumia sabuni na maji safi na utumie taulo kujikausha.
Ingawaje jambo hili linaweza kuwa gumu kwa wanaoishi kwenye makazi duni, na
walio vijijini ambako maji safi hayapatikani kirahisi, lakini ni mbinu
iliyothibitishwa kuweza kuua virusi vya ebola.
Pia wataalam wanashauri kusalimiana
kwa mikono kuepukwa kwa ujumla.
Dk Unnis Krishnan wa Plan International
aliarifu BBC, kuwa ebola husambazwa haraka watu wanapowasiliana ana kwa ana na
maji maji ya kimwili ya waliougua. Hivyo ni vizuri kutumia njia nyingine za
kujuliana hali.
2. Hakuna kugusana
Iwapo unashuku kuwa mtu ana ebola,
usimguse. Ingawaje inaweza kuonekana kuwa si maadili mema unapoona unaowapenda
wakihisi uchungu na unataka kuwakumbatia na kuwahudumia, lakini haiwezekani.
3. Epuka miili ya wafu
Iwapo unadhani mtu amefariki baada
ya kuugua ebola, usiguse mwili wao, hata kama ni mila au desturi ya maziko. Hii
ni hatari kwa sababu baada ya mtu anapofariki bado huweza kuambukizwa ebola
kutoka kwa miili yao kwani bado inatoa maji maji ya mwili, ambayo huweza kuwa
hatari zaidi.Ni vyema kufanya mipango ya kupata timu ya magwiji kushughulikia
mwili huo haraka iwezekanavyo kwani ni hatari kuacha mwili wa mfu kwa muda
mrefu katika eneo la makazi.
4. Usile nyama ya porini
Epuka kuwinda, kugusa, au kula nyama
ya porini, kwa mfano popo, nyani na sokwe, kwani wanasayansi wanaamini kuwa
hiyo ndiyo chanzo cha maambukizi kwa binadamu.
Pia wataalam wanashauri hata kama
mnyama fulani wa porini huliwa katika eneo lenu na nyama yake ni tamu ni vyema
kuepuka myama huyo kwani nyama yake au damu huweza kuwa na virusi hivyo.
Hakikisha vyakula vyote vinapikwa inavyostahili.
5. Usiwe na hofu
Kueneza uvumi huongeza hofu. Usiogope
wafanyakazi wa huduma za afya, pia usiamini matibabu ya kiasili ambayo
hayajathibitishwa kutoa afueni, kwani suala hilo limechangia sana ongezeko la
kuenea kwa virusi vya Ebola katika nchi zilizoathirika.
Mtu huweza kupata maambukizi ya
ugonjwa huu endapo utagusa maji maji ya kimwili- mkojo na kinyesi, matapishi,
kamasi, mate, machozi, na mbegu za kiume na majimaji ya uke- vyote huweza
kueneza ebola endapo mhusika atakuwa ameathirika na ugonjwa huo.
Dalili za mtu aliyeugua ni joto
mwilini, maumivu ya misuli na viungo, vidonda kooni, kuumwa na kichwa, na
uchovu, kufuatiwa na kichefuchefu, kutapika na kuharisha, ambapo mtu huweza
kutoa damu pia. Ebola bado haina tiba sasa. Na BBC
No comments:
Post a Comment