Kushoto ni mwandishi wa TABIBU akizungumza na Mzee Maulid alipomtembelea nyumbani kwake Mbagala Kongoe (Picha na mwandishi wetu) |
- · Kwa sasa anakojoa kupitia mirija
- · Awaomba Watanzania kumsaidia na ikiwezekana aonane na JK
Mzee Maulid
Kakonda mkazi wa Mbagala Kokongoe jijini Dar es Salaam amekuwa akiteseka na
maradhi ya kibofu cha mkojo tangu mwaka 2012 na kupelekea kuishi na maumivu
makali katika maisha yake tangu kukubwa na maradhi hayo.
Akizungumza
na TABIBU hivi karibuni, Mzee Maulid anasema kuwa maradhi hayo yalianza
kumsumbua mwaka 2012, ambapo alijikuta akianza kupata haja ndogo kidogo sana
(mkojo), pamoja na maumivu makali na baadaye alishindwa kabisa kupata mkojo.
“Kwenye siku mbili tatu niliona mkojo
unatoka kidogo sana na baadaye ukabana zaidi na kuacha kabisa kutoka,” alisema
mzee Maulid.
Baada ya hali
hiyo mzee Maulid anasema alilazimika kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili,
ambapo madaktari waligundua alikuwa anasumbuliwa na tatizo la uvimbe kwenye
kibofu na kupelekea kufanyiwa upasuaji na kuwekewa mirija miwili ambayo ndio
inamsadia katika kutoa haja ndogo kwa sasa.
Kutokana na
hali hiyo mzee huyo anasema kwa sasa kila baada ya wiki mbili huwa anakwenda hospitali
kubadilisha mirija, ambapo anasema mara nyingi anapobadilishwa mirija hiyo
hupatwa na maumivu makali ambayo mara nyingi humsababishia homa kali.
Mzee Maulid,
anasema tangu alipoanza kusumbuliwa na maradhi hayo amekuwa akipatiwa matibabu
bure, baada ya kupata msamaha wa matibabu, ambao aliupata kutokana na juhudi za
Serikali yake ya mtaa, lakini kwa sasa anasema muda wa msamaha huo umekwisha,
hivyo anahitajika kutoa pesa ili kuweza kuendelea na matibabu zaidi hususani
upasuaji mwingine wa pili.
Hapo awali
kabla ya maradhi hayo mzee Maulid, anasema alikuwa akipata ridhiki kupitia kuchukua
magazeti yaliyokwisha somwa katika ofisi mbalimbali, kisha kuyauza kwa wamiliki
wa maduka, ambayo hutumika kufungia bidhaa mbalimbali. Lakini kwa sasa kutokana
na maradhi yake hayo amekuwa akishindwa kufanya shughuli hizo hivyo kupelekea
maisha ya familia yake yenye jumla ya watu 6 kuwa katika hali ngumu zaidi.
“Maisha
yangu bado ni ya shida kwa sasa, kwa sababu hapa nilipo bado sijajua lini nitapata
uzima, lakini naamini kwa uwezo wa mwenyezi Mungu madaktari watanifanyia
huduma,” alisema Mzee Maulid.
Mbali na
maradhi hayo mzee Maulid pia anatatizo la ulemavu, ambapo anasema ulemavu huo
aliupata kupitia kwa waganga wa jadi, baada ya kukupwa na ganzi mwilini, tatizo
lililompelekea kwenda kwa waganga wa jadi ambako alikuwa akipatiwa matibabu ya
tatizo hilo kwa njia ya kuchua.
“Mimi nilizaliwa mzima kabisa, lakini
matatizo haya ya miguu yametokana na waganga wa jadi, ambao walikuwa wakinichua
sana pindi nilipokuwa nikisumbuliwa na ganzi mwilini, lakini kumbe walikuwa
wananichua kwa nguvu nyingi sana na mwishowe nilijikuta nikiwa katika hali hii
unayoniona nayo,” alisema Mzee Maulid.
Pamoja na
hayo, mzee huyo amewaomba Watanzani kumsaidia ili aweze kuendelea na matibabu
yake, lakini pia ameomba kusaidiwa kutokana na hali ngumu ya maisha yake anayoipitia
kwa sasa yeye pamoja na familia yake.
Hata hivyo,
Mzee Maulid alisema kuwa angefarijika sana endapo angefanikiwa kuonana na Rais
Jakaya Mrisho Kikwete kwa lengo la kumuelezea matatizo aliyonayo hususani juu
ya maradhi yake hayo.
“Unamuona kijana yule aliyeungua
moto, alisaidiwa sana na Mheshimiwa Rais Jakaya, hivyo na mimi nilikuwa
namuomba mheshimiwa rais nimuone kwa hali na mali, ili nimuelezee shida
niliyoipata na matatizo yangu ana kwa ana ili na mimi anisaidie maana najua
tatizo langu hili anaweza kunisaidia,” alisema Mzee Maulid kwa kusisitiza sana.
Naye Abdala
Mpanjinji ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mzinga kata ya Tuangoma
wilaya ya Temeke amekiri kumfahamu mzee Maulid mtaani hapo na namna anavyokabiliwa
na matatizo ya maradhi yake hayo.
Hata hivyo, Mpanjinji
amesema wamekuwa wakimsaidia kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya
matibabu yake, ambapo walimsaidia kumuandikia barua kwa Mganga Mkuu wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo barua hiyo ilimsaidia kupatiwa matibabu
bure tangu mwaka 2012.
Aidha,
Mpanjinji ameongeza kuwa kwa sababu muda wa msamaha wa matibabu umeshakwisha
kwa sasa, lakini bado wao wapo tayari kumuandalia barua nyingine
itakayomuwezesha kumsaidia kuendelea kupata matibabu kwa msamaha.
Madaktari wanasemaje kuhusiana na
matatizo ya kibofu cha mkojo?
Daktari
kiongozi wa Hospitali ya Amana Dk. Gilbert Ngua aliliambia TABIBU kuwa ugonjwa
huu huweza kusababishwa na mambo mengi na kitaalamu huitwa ‘bladder Outlet Obstruction’ (BOO).
Dk. Ngua
anasema miongoni mwa mambo yanayoweza kupelekea matatizo katika kibofu cha
mkojo ni pamoja na kuvimba kwa tezi dume (prostate hyperplasia), mawe kwenye
mfuko wa mkojo (bladder stones), magonjwa ya zinaa hususani kisonono, makovu
(urethral scars), vichocheo (hormones) pamoja na umri nk.
Aidha, Dk.
Ngua alizataja dalili za tatizo hili kuwa ni pamoja na kupatwa na maumivu chini
ya kitovu, kukojoa mara kwa mara hasa usiku, kujisikia kibofu kujaa muda wote,
tumbo kujaa hasa chini ya kitovu, kupata shida wakati wa kukojoa (hesitancy),
kujikojolea (incontinence), sambamba na mkojo kukosa nguvu (weak stream).
Hata hivyo,
daktari anashauri watu kwenda hospitali kupima ili kujua chanzo cha tatizo,
huku akisema tiba ya tatizo hilo hutegemea chanzo na mara nyingine upasuaji
huweza kuhitajika.
Wataalam wa tiba asilia wanasemaje?
Dk.Geoffrey
Lusanzu, ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Tanamerec Herbal Clinic kilichopo
Kabanga wilayani Kasulu mkoani Kigoma naye anasema sababu huwa ni
matatizo ya tezi dume, ambapo tezi hizo huweza kuharibika
ama kwa kukonda au kupanuka.
Dk. Lusanzu
anasema hali ya kupanuka hufanya tezi dume kulalia mirija ya mkojo na hivyo
kuifanya mirija hiyo ipinde na kusababisha mkojo kushindwa kupita kirahisi.
Hata hivyo, naye
anasema kuwa kwa kawaida hali hiyo husababishwa na maambukizo ya
wadudu wa maradhi au hali ya umri wa uzee hususani kuanzia miaka 50 na kuendele.
Huku akiongeza kuwa tiba asilia zina nguvu kubwa ya kutibu tatizo hilo kwa muda
wa wiki 4 tu.
Kwa habari kama hizi na nyingine nyingi hakikisha hukosi nakala yako ya TABIBU kila siku ya Alhamisi kwa shilingi 500/= tu
No comments:
Post a Comment