Na
Seif K. Oddo
Ni ukweli
usiopingika, japokuwa tuliowengi hatufahamu ya kwamba magonjwa mengi
yanayosumbua miili yetu tunajitengenezea au kujisababishia sisi wenyewe. Miili
yetu imeumbwa ili iweze kutumika katika kiwango fulani, hivyo kuitumia chini au
juu ya kiwango hicho husababisha magonjwa mbalimbali.
Maendeleo ya teknolojia yameleta starehe au raha na
kurahisisha maisha kwa kiasi kikubwa, ila nyuma ya maendeleo haya ya teknolojia
yamebeba athari za kiafya katika miili yetu bila ya sisi kufahamu. Kwa mfano
watu wengi kwa sasa wamekuwa wakipenda kutumia magari katika matembezi, tena
hata kwa umbali mdogo, watu wengi hupenda kuketi kwa muda mrefu majumbani
wakiangalia tamthilia katika televisheni zao. Walio wengi wanapenda kufanya kazi
zisizotumia nguvu hata kidogo, pia watu wengi hupenda kutumia lifti kupanda
katika majengo marefu wanapokwenda maofisini mwao.
Mfumo huu wa
maisha ya aina hii ndio hasa unaopelekea tushindwe kutumia miili yetu ipasavyo
pamoja na virutubisho tunavyokula katika vyakula mbalimbali. Miili yetu haihitaji
kiasi kikubwa cha virutubishi hivi na visipopunguzwa hurundikana na kuwa sumu
ambayo husababisha magonjwa mbalimbali kama vile kisukari, saratani na magonjwa
mengineyo.
Hapo ndipo umuhimu wa kufanya mazoezi unapochukua
nafasi kubwa katika kulinda na kuimarisha afya ya binadamu. Mazoezi ni tiba na
pia ni kinga ya mwili wa binadamu dhidi ya magonjwa mbalimbali.Kupitia mazoezi,
tunaweza kupunguza mafuta na kuondoa baadhi ya sumu ndani ya miili yetu na hata
kupunguza uzito wa mwili ambao pia huwa ni kikwazo kiafya.
Hivyo basi tunashauriwa kufanya mazoezi mara kwa mara
ili kuimarisha afya za miili yetu. Ni vyema mtu akatenga muda maalum kwa ajili
ya kufanya mazoezi, kama unavyotenga muda maalum kwa ajili ya kula. Inashauriwa
mbali na kutenga muda huu, pia ni lazima kuheshimu kwa kufuata ratiba ya
mazoezi uliojipangia ili kufikia lengo. Kuna baadhi ya sehemu za miili yetu hazitibiki
kwa dawa au kwa upasuaji isipokuwa kwa mazoezi pekee. Hivyo basi mazoezi ni
kitu muhimu sana kuliko watu wengi wanavyodhani.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, imebainika kuwa kwa
kufanya mazoezi unawezesha mwili kutumia virutubisho ipasavyo, kwani hakutokuwa
na kinachohifadhiwa ama kubaki mwilini kinyume na matakwa ya mwili.
Sio lazima mtu ufanye mazoezi magumu sana, kuna aina
tofauti za mazoezi ambayo unaweza kuyatumia kwa afya. Kwa mfano kutembea umbali
mrefu, kukimbia taratibu kwa umbali mrefu, kuendesha baiskeli na mazoezi ya
viungo.
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Karolinska nchini
Sweden, wamebainisha katika tafiti zao kwamba kutembea kwa kawaida kwa muda wa
saa moja kwa siku, kwa muda wa siku tano kunaweza kushusha kiwango cha sukari
kwa wagonjwa wa kisukari na kufikia kiwango cha kawaida kwa asilimia zaidi ya
sabini.
Utafiti uliofanywa na wanasayansi kutoka Chuo Kikuu
cha Sayansi za Tiba cha Muhimbili, hapa nchini umeonesha kwamba watu wenye
tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara, wana kinga zaidi ya kutopata maradhi ya
kisukari na moyo ukilinganisha na wale wasiofanya mazoezi kabisa.
Mbali na hayo, tafiti zimeonesha jamii zinazoishi
vijijini na kujishughulisha na kilimo pamoja na ulaji wa vyakula vya asili
ikiwemo kujishughulisha na shughuli zinazotumia nguvu, zimekuwa na kiasi kidogo
sana cha magonjwa ya kisukari, moyo na saratani ikilinganishwa na jamii
zinazoishi maisha tunayoyaita ya kisasa, ambapo watu hawapendi kabisa kusumbua
miili yao.
Ikumbukwe kwamba mazoezi yanatambuliwa kama dawa
katika nchi mbalimbali, mazoezi yana uwezo mkubwa wa kuzuia kisukari, ugonjwa
wa moyo, unene wa kupindukia, saratani, magonjwa ya viungo, msongo wa mawazo na
magonjwa ya mfumo wa homoni. Hakika kinga ni bora kuliko tiba, gharama ndogo
itakayokugharimu kwa kufanya mazoezi, sio sawa na gharama kubwa itakayokukumba
kwa kutibu magonjwa ambayo ungeweza kuyadhibiti kwa kufanya mazoezi tu.
Ni ngumu kuamini kwamba wakati mwingine unaweza
kujiepusha na kifo kwa kufanya mazoezi, kwani watu wengi hupoteza maisha kwa
kushambuliwa na magonjwa ambayo wangeweza kuyadhibiti na kuyaepuka kwa kufanya
mazoezi, hapo unaweza kuona ni kwa kiasi gani mazoezi yalivyo muhimu katika
maisha yako.
Baadhi ya watu wanadhani mazoezi ni kwa ajili ya
kutengeneza maumbo mazuri ya miili tu, wengine wanaamini mazoezi ni kwa ajili
ya watu wanene tu. Ukweli ni kwamba, mbali na kutengeza maumbo mazuri ya miili,
lakini pia hata watu wasio na miili minene wanapaswa kufanya mazoezi kwani
mazoezi, yanaboresha afya na kusaidia kuzuia magonjwa hatari mwilini.
Kwa wale wanaopenda kutumia lifti kuelekea katika
ofisi zao, ni vyema wakatumia ngazi badala ya lifti au tumia lifti hadi ghorofa
chache kabla ya kufika katika ghorofa
uendayo, kisha shuka kutoka katika lifti na umalizie kwa kupanda ngazi mbaka
ufike unapoelekea.
Na kwa wale wanaotumia usafiri mara kwa mara, ni vyema
ukatafuta sehemu ya umbali wa kiasi uliegesha gari lako, kisha tembea kwa miguu
hadi ofisini kwako na endapo unafanya kazi zisizotumia nguvu, jitahidi kwa kiasi
fulani kufanya kazi ukiwa umesimama, ili kuepuka kukaa kwa muda mrefu, ambapo
itakusaidia kuepuka matatizo ya uti wa mgongo, na badala yake simama na
tembeatembea hapo ofisini.
Wataalam wa masuala ya afya wanashauri kunywa maji
ya kutosha baada ya kufanya mazoezi, kwa wale wanopenda kufanya mazoezi magumu
kama vile kunyanyua vyuma vizito, inashauriwa kupata ushauri wa daktari kabla
ya kuanza mazoezi hayo.
Nakushauri ndugu Mtanzania msomaji wa blog hii ya TABIBU,
kama hujaanza mazoezi anza sasa na ukumbuke mwili wako ni kitu chenye thamani
kubwa kuliko kitu kingine chochote hapa duniani.Hivyo basi, kuulinda mwili wako
ni jukumu lako. Epuka kujibweteka na uanze kuupa mwili mazoezi ya kutosha ili
kujenga afya bora. Kumbuka, mazoezi ni tiba.
No comments:
Post a Comment