Tangawizi imezoeleka kutumika kama kiungo katika vyakula vya aina mbalimbali. Baadhi ya watu hutumia katika chai ili kuongeza ladha.
Hapa nchini tangawizi hulimwa sana maeneo ya nyanda za juu kusini na baadhi ya mikoa kama vile Kilimanjaro, Manyara na Morogoro.
Kiungo hiki hupatikana kwa wingi katika masoko mbalimbali jijini Dar es Salaam na mara nyingi huuzwa kwa bei na fuu, hivyo basi kila mtu anauwezo wa kumudu kununua kiungo hiki adhimu.
Miaka 500 iliyopita tangawizi ilitumika nchi za mashariki ya mbali hususani China na India kwa kutibu maradhi mbalimbali. Aidha, tafiti zilizofanywa na wataalamu wa masuala ya tiba za asili zimebainisha kwamba, kiungo hiki kinauwezo wa kutibu magonja zaidi ya 72. Huku wakibainisha kwamba ndani ya tangawizi kuna magnesium, potassium, copper na vitamin B6.
Mbali na hayo, wataalamu wanaeleza kuwa ndani ya tangawizi kuna ‘Volatile Oil,’ ambayo ni kiasi cha asilimia 25 hadi 30. Ndani ya ‘Volatile Oil,’ kuna ‘Ginger Oil’ ‘terpene,’ ‘ginger phenol’ na ‘Camphorterpene.’ Huku wataalamu wakieleza kuwa ‘Volatile Oil’ inafanya kazi ya kusaidia damu itiririke haraka mwilini, jambo ambalo hufanya chembe hai mwilini kuchapa kazi vizuri zaidi. Pia wataalamu wanaeleza kuwa ndani ya tangawizi kuna ‘pungent’ kwa kiasi cha asilimia 1.5, ambayo huifanya tangawizi kuwa na ladha ya ukali, pungent hiyo husaidia kuyapatia matumbo yetu nguvu.
Tangawizi inapotumika kikamilifu huweza kutibu maradhi ya maumivu ya tumbo, ambapo hutuliza maumivu hayo yanayosababishwa na matatizo ya usagaji wa chakula. Pia huongeza hamu ya kula na huondoa gesi tumboni.
Hali kadhalika kiungo hiki husaidia kuondoa maumivu ya gauti na pia huzuia kuganda kwa damu mwilini na husaidia kusambaza damu mwilini kwa urahisi.
Aidha, tangawizi huweza kutumika kuondoa kichefuchefu kinacho sababishwa na hali ya ujauzito. Huku ikibainika kupunguza mafuta mwilini na hivyo kusaidia kuondoa maradhi ya moyo. Mbali na hayo kiungo hiki pia husaidia kutibu maumivu ya koo na kukauka kwa sauti.
Pamoja na hayo, wataalamu wa tiba za asili wanaeleza kuwa tangawizi ikitumika kwa kuchanganywa na asali huweza kuondoa na kuponya mafua, pumu pamoja na kufungua mfumo wa upumuaji.
Pia tangawizi huweza kutumika kama tiba ya kuongeza nguvu za kiume na tatizo la wanaume kuwahi kufika kileleni wakati wa tendo la ndoa, mbali na hapo pia hutumika kama tiba katika kutibu tatizo la vijiwe kwenye figo.
Imefika wakati sasa kwa watanzania kupenda au kujijengea mazoea ya kula vyakula vya asili na kuepuka kupenda kutumia vyakula vya viwandani kwa wingi, ambavyo uandaaji wake uhusisha na matumizi ya kemikali ambazo husababisha sumu katika miili yetu.
Imekua kama ni kawaida au kama kwenda na wakati kwenda katika ‘super markets’ kununua vyakula vilivyosindikwa kutoka nje ya nchi, ikiwemo nyama za kwenye makopo, samaki na hata matunda, ambayo yamekaa muda mrefu bila kuharibika. Kwa upande wangu sishauri mwenendo huu, iweje ukanunue tunda lililokaa mwezi mmoja bila kuharibika wakati uwezekano wa kupata tunda hilo sokoni, ambalo bado lipo katika hali yake ya asili bila hata ya kuhifadhiwa kwa kemikali ya aina yoyote upo. Hivyo ni vyema kwenda na wakati kwetu kusitufanye tukasahau kutumia vyakula vya asili, ambavyo ni salama zaidi kwa afya zetu.
Sambamba na hayo, ni vizuri tukafahamu kwamba matumizi ya tangawizi pekee, huweza kutupatia faida lukuki, hivyo ni vizuri kama tutajijengea mazoea ya kutumia kiungo hiki katika chai na hata katika vyakula vingine kama vile nyama, kwani tangawizi pia huifanya nyama kuwa laini na kuiva vizuri. Kumbuka kwamba vyakula vya asili ni tiba, anza sasa kutumia tangawizi kwa afya yako.
No comments:
Post a Comment