Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Tuesday, December 16, 2014

Vidonda vya tumbo Kushnei
Na Juma Diwani
Haipingiki kuwa ugonjwa wa vidonda vya tumbo ni miongoni mwa magonjwa yanayoisumbua jamii kwa kiwango kikubwa.

Vidonda vya tumbo ni nini
Vidonda vya tumbo (peptic ulcers) ni matokeo ya kuharibika kwa uteute wa ndani ya ukuta wa tumbo la chakula au katika utumbo mdogo na hivyo kusababisha ukuta wa tumbo kugusa tindikali iliyoko tumboni ambayo ni kali na mwishowe kupelekea vidonda.


Vidonda hivyo huweza kujitokeza katika utumbo mdogo au katika tumbo la chakula na nadra sana huweza kujitokeza kwenye koromeo la chakula ambako huwa hakuna uwezo wa kustahimili tindikali ya tumboni.

Hata hivyo, tafiti zinaonesha kwamba ugonjwa huu wa vidonda vya tumbo unaelezwa kusababishwa na kimelea jamii ya bakteria aitwaye ‘Helicobacter pylori (H. Pylori)’ ambaye huweza kusababisha asilimia 90 ya vidonda vya tumbo katika utumbo mdogo na asilimia 80 katika tumbo la chakula.

Hali hii husababishwa zaidi na kushindwa kwa mfumo wa kinga mwilini kuwaua na kuwaondoa kabisa vimelea hao wa H. Pylori ndani ya mwili. Hivyo matokeo ya kushindwa huko husababisha kuwepo kwa maambukizi ya kudumu katika kuta za tumbo (chronic active gastritis),
Maambukizi hayo huharibu mfumo na uwezo wa kuta za tumbo kutunza vichocheo vya ‘gastric hormones’ ambavyo ni muhimu katika kuhakikisha mazingira ya tumbo yanakuwa na kiwango salama cha tindikali.

Kwa kawaida, kazi ya ‘gastric hormones’ ni kuchochea utolewaji wa tindikali ‘gastric acid’ kutoka kwenye seli za ukuta wa tumbo zijulikanazo kama ‘parietal cells’ na iwapo bakteria hawa watashambulia na kuharibu ukuta wa tumbo, mfumo wa gastric pia utaharibika. Hii inasababisha vichocheo vya ‘gastric’ kuzalishwa kwa wingi hali ambayo pia huchochea uzalishaji wa ‘gastric acid’ kwa wingi. Matokeo ya kuzalishwa kwa wingi kwa tindikali hiyo hupelekea kuchubuka kwa ukuta wa tumbo na hivyo kusababisha vidonda vya tumbo.
Kuna aina kuu mbili za vidonda vya tumbo. Aina ya kwanza ni ile inayoathiri tumbo ‘gastric ulcers’ na aina ya pili ni vile vinayotokea kwenye sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo ambapo kitaalamu huitwa ‘duodenal Ulcers’. Aina zote mbili kwa pamoja huitwa ‘peptic ulcers.’

Madaktari wanasemaje kuhusu tatizo hili?
TABIBU ilifanikiwa kuzungumza na Dk. Alex Shuli kuhusiana na tatizo hili ambapo alisema kuwa Watanzania wengi wanasumbuliwa na vidonda vya tumbo na kubainisha baadhi ya sababu zinazopelekea kutokea kwa tatizo hilo ambazo ni pamoja na matumizi ya muda mrefu ya dawa za kuondoa maumivu za kundi la ‘Non Steroid Anti-inflammatory Drugs(NSAIDs) kama vile Diclofenac, Aspirin, Ibuprofen na Diclopar, msongo wa mawazo na unywaji wa pombe kupitiliza. Hata hivyo, unywaji wa pombe sambamba na maambukizi ya vimelea vya ‘Helicobacter Pylori’ huongeza madhara ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo.

Aidha, Dk. Shuli alifafanua miongoni mwa dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kutapika na wakati mwingine kutapika damu, kupatwa na kiungulia, kukosa hamu ya kula au mgonjwa kupata haja kubwa yenye rangi nyeusi pamoja na kupata maumivu sehemu ya chemba ya kifua.
Vidonda vya tumbo huweza kubainika kwa kutumia kipimo kiitwacho endoscope,’ ambapo daktari huangalia moja kwa moja ndani ya utumbo wa mgonjwa ili kuona sehemu iliyo na vidonda pamoja na ukubwa wa tatizo lake.
Pia vipimo hivi humwezesha daktari kuchukua sehemu ya utumbo iliyoathiriwa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara zaidi ili kutambua endapo ni vidonda vya tumbo pekee au kuna tatizo lingine.
Pamoja na kuwepo na imani kwamba maziwa huweza kutibu vidonda vya tumbo, lakini wataalam wa afya wanasema kwamba maziwa huweza kumfanya mtu kujisikia ahueni tu na si kupona kabisa, huku wataalam hao wakisema kuwa maziwa huongeza tindikali ‘acid’ tumboni ambayo huweza kuleta madhara makubwa ya vidonda tumbo.
Miongoni mwa dawa ambazo huweza kusaidia tatizo la vidonda vya tumbo ni pamoja na ‘Omeprazole’ na ‘Mucogel.’ HIzi hushauriwa mgonjwa kutumia mara apatapo ushauri kutoka kwa madaktari au wataalam wa madawa kabla ya kuanza kutumia dawa hizo ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza pale zinapotumiwa pasipo maelekezo ya wataalam hao.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasemaje
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), imethibitisha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu duniani wanavimelea vya ‘Helicobacter pylori’ katika utumbo, ingawa miongoni mwao karibu asilimia 80 hawaoneshi dalili yoyote ya kuugua.
Watanzania wanalizungumziaje tatizo hili
TABIBU ilifanya mahojiano na wakazi wa Dar es Salaam ambao asilimia sabini kati yao walisema kuwa tatizo hili ni hatari ambalo linawasumbua ingawa hawana ufahamu na taarifa za uhakika kuhusiana na tatizo hilo wakati asilimia thelathini walisema hawajui.
Hata hivyo, wengi wao walidai kuwa wanaume wengi wanaathirika zaidi na tatizo hilo kutokana na kuwa na majukumu mengi ya familia yanayowapelekea kusongwa na mawazo juu ya namna ya kuzihudumia familia zao.
Wataalam wa tiba asili wanasemaje?
TABIBU ilifanikiwa kumtafuta mmoja wa wagunduzi wa kwanza wa dawa ya vidonda vya tumbo nchini Tanzania anayefahamika kama Dk. Rahabu Lubago kutoka Rahabu Ulcers Clinic Centre. Kituo chake kinapatikana jijini Dar es Salaam na kilifanikiwa kugundua dawa hiyo tangu mwaka 1998 iitwayo ‘Fiterawa.’ Dawa hii imeonekana kuwa msaada mkubwa kwa Watanzania wengi juu ya matatizo ya vidonda vya tumbo.

Mtaalam huyo wa tiba asilia nchini, alisema kuwa vidonda vya tumbo hutibika kupitia tiba asili bila shaka yoyote endapo mtumiaji atazingatia masharti na matumizi ya dawa na kuitaja dawa ambayo ina uwezo wa kutibu ugonjwa huo.
“Vidonda vya tumbo vinatibika na kutorejea tena wakati mgonjwa atakapotumia ‘Fiterawa’ na kuzingatia masharti na matumizi ya dawa hii,” alisema Dk. Rahabu.
Masharti ya vyakula wakati wa matumizi ya dawa hiyo ya asili
Dk. Rahabu alisema kuwa mgonjwa anapaswa kuzingatia vyakula katika kipindi hiki, huku akisema kuwa mgonjwa hapaswi kula maharage au nafaka yoyote au nyanya, pilipili, ndimu, mchicha, kisamvu, majani ya kunde, ndizi aina zote, mayai, chipsi, nk.

Huku akibainisha matunda yasiyofaa pia katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na maembe, machungwa, mapesheni, machenza na matunda yenye tindikali au yanayozalisha gesi.

Masharti mengine ni kuacha kunywa pombe au soda ya aina yoyote.

Hata hivyo, katika kipindi hiki epuka vinywaji baridi sana, mtindi, uji wa ulezi, majani ya chai, kahawa, magadi pamoja na kutotumia dawa zenye tindikali. Hali kadhalika, katika wakati huu mgonjwa hapaswi kuvuta sigara wala kutumia ugoro, kuberi na tumbaku.

No comments:

Post a Comment