Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Tuesday, December 16, 2014

Tushirikiane kutokomeza UKIMWI

Na Juma Diwani
Tatizo la UKIMWI si geni masikioni mwa watu kwani huripotiwa mara kwa mara katika vyombo vya habari, tatizo ambalo husababisha vifo bila kujali rangi wala kabila huku likiongeza umaskini, idadi ya mayatima na watoto wa mitaani.


Aidha,kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa kuwa watu kati ya milioni 1.4 hadi 1.7 walifariki dunia kutokana na tatizo hilo mwaka 2013.

Wengi wetu tumeshashuhudia jinsi ndugu zetu walivyopoteza maisha yao kutokana na ugonjwa huu. Tunaweza kusema hakuna hata familia moja au mtu yeyote kati yetu Watanzania anayeweza kusema kuwa hajaguswa na athari mbaya za UKIMWI na kama yupo basi ni wa kutazamwa kwa mshangao usiopimika.

Wanaokufa kwa UKIMWI ni nguvu kazi ambayo inaondoka duniani huku mchango wao ukiwa bado unahitajika. Tunasema hivyo tukiamini kabisa kuwa wengi wa wanaokufa kwa UKIMWI kwa sasa ni wasomi, vijana na watu wenye nguvu motomoto katika kutenda.

Inatia moyo hasa kuona kuwa, viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali hadi kitaifa, wameivalia njuga vita dhidi ya UKIMWI na kuweka mikakati mbalimbali kupigana na ugonjwa huu.

Hata hivyo, bado inasikitisha kwani licha ya juhudi hizo zikiwemo za elimu ya mara kwa mara juu ya UKIMWI, bado ugonjwa huu hatari unazidi kushamiri.

Hata hivyo, yapo mambo mengi yatupasayo kufanya ili kuondokana na ugonjwa huu mbaya lakini kubwa zaidi, tukae chini tuulizane kuwa, ‘kwa nini UKIMWI unazidi kushamiri? Sababu hasa ni nini, nasi tunashindwa wapi? Sasa, kila mmoja afanye nini?’

Huku nyumba za kulala wageni zikielezwa kuwa kichocheo cha tatizo hili, mara nyingi nyumba hizi hutumiwa hata na watu wasiofahamiana kwa muda mrefu ambao huchukuana kiholela na kwenda huko kufanya uzinzi katika nyumba hizo.

Wakati huo huo, gesti nyingi zipo pamoja na baa za vinywaji mbalimbali kama bia na pombe za aina nyingi. Hapo ni vema kila mmoja akumbuke na kuzingatia kuwa kwa asilimia kubwa ya uzinzi na ulevi ni marafiki wakubwa na ndiyo maana kila alipo bwana ulevi si rahisi kumkosa bwana uzinzi.

Hivyo, ni rahisi kwa mtu aliyelewa pombe kutamani kufanya mapenzi na mtu yeyote, bila kufikiria kwa makini, hata kama hamjui, bila woga kwa Mungu na bila aibu kwa watu. Huu ni ukweli ulio bayana.

Binadamu ni kiumbe mwenye akili na utashi, na hivyo akili yake ndiyo inayotawala mwili, lakini kama inatokea kuwa vionjo vya mwili ndivyo vinavyotawala akili basi huyo si binadamu tena aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu.

Kwa kadiri ya akili ya binadamu akiambiwa kuwa kuna hatari mahali fulani, hujiweka katika tahadhari ili hatari isimpate, lakini cha kushangaza ni katika ugonjwa huu. Ingawa elimu kadha zinatolewa dhidi yake, tunashuhudia namna wengi wetu wanavyoendelea kupuuzia jambo hilo.

Sote tunapaswa kujua kuwa huo ni ugonjwa ambao kwa kweli unadaiwa hauna tiba bali, una kinga ambayo siyo hasa kondom, bali ni utashi wake binadamu wa kujishinda katika kufanya vitendo vya ndoa nje au kabla ya ndoa.

Katika hatari mbalimbali ambazo binadamu hukumbana nazo, mara nyingine huona kimakosa kuwa kitu fulani ni kinga itakayomsaidia, kumbe sivyo.

Tunao ule msemo usemao, ‘kufa kufaana’ hivyo yawezekana kuwa hata katika janga la UKIMWI, kuna kufa kufaana, yaani kuna watu wanaofaidika kutokana na balaa hilo.

Tunapaswa kuwa waangalifu sana katika kupokea ushauri na hata hizo zinazodaiwa kuwa ni kinga za nguvu. Ni lazima tutambue kuwa hapo kuna vitu vya biashara pia, licha ya kudaiwa kuwa ni misaada ya kutuonea huruma sisi wananchi.

Tumesikia kuwa kuna mikoa inayosifika kwa utumiaji wa kondom, lakini bado hatujaambiwa kwamba hiyo mikoa imepunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa kiasi kipi.

Wengi wetu tumekuwa tukisikia kwamba wenzetu wa Uganda wamefanikiwa kupunguza kasi ya UKIMWI siyo kwa sababu waligawiwa na kutumia kondom, bali kwa sababu walikubali kubadili tabia zao.

Kanuni yetu iwe ni ile ya wanausalama, kwamba tusimwamini kila mtu na tumtilie mashaka kila mtu. Haifai kusema kuwa mtu huyu ni salama ama sivyo kwa mtazamo wa macho matupu.

Pia, tusijidanganye kwa kuwaamini wanaodai kupimwa na kuonekana salama siku hiyo kwani cheti hicho si cha kudumu.

Yawezekana kuwa aliyekuwa salama juzi, leo anaweza kuwekwa katika kundi la waathirika hivyo, kinachotakiwa ni kuwa imara katika kuilinda miili yetu.

Hatimaye, tunapaswa kufahamu kuwa UKIMWI upo huku ukizidi kutokomeza watu na ni hatari tushirikiane kuutokomeza.

No comments:

Post a Comment