Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Tuesday, December 16, 2014

Kuathirika kisaikolojia 
Na John Chikomo
1.     UTANGULIZI
Watu wengi wamekuwa wakitumia neno Matatizo ya kisaikolojia katika maisha ya kila siku wakimaanisha hali ya mtu mwenye tabia na mwenendo tofauti katika jamii. Lakini ufunguo wa kujua matukio ya matatizo ya kisaikolojia  ni hali ya mtu kuwa na msongo mkubwa wa mawazo ambayo mtu anashindwa kukabiliana nayo. Wataalam mbalimbali katika taaluma wanaelezea matatizo ya kisaikolojia katika mitazamo mbalimbali.
Ninachojaribu kukikazia katika somo hili ni kwamba mtu binafsi ndiye anayeweza kuelezea vizuri kuwa tukio lililompata limemuumiza au lah.
2.     Hivyo tafsiri ya kuathirika kisaikolojia ina mapana yake, inajumuisha miitikio yenye nguvu ya matukio mengi ya kuumiza kama; ajali, majanga asilia, ukatili, kufanyiwa upasuaji, umaskini, kuachika/kuachana, magonjwa, kukataliwa na mzazi, kubakwa, uharifu wa kutumia silaha, mafuriko, kukosa ajira, kufiwa na mpenzi, ulemavu na, kutukanwa.
Moja kati ya watu niliowahi kuzungumza nae, akiwa katika kujieleza yanayomsibu alisema “Baada ya jambo hili kunitokea nilijihisi kama nimetwishwa mzigo mkubwa sana kichwani kwangu, muda wote”
Pamoja na kwamba matukio yote hayo yaliyotajwa hapo juu yanaumiza, lakini lakini siyo yote huitwa kuathirika kisaikolojia. Lakini mengine huitwa mapitio ya kisaikolojia (Traumatic experiences), na mapitio haya ya kisaikolojia huwa inakuwa ya ghafla na ya-kushtua, na inahusisha hatari na hisia ya woga, na kukosa matumaini.
Kwa Mfano, mama mmoja tukiwa katika mazungumzo, mbali na mambo mengi aliyoelezea akijaribu kuonyesha hatua aliyofikia alisema “nilidhani huo ndio ulikuwa mwisho wa maisha yangu, nisingewaona tena wanangu”.
Tofauti kati ya kuathirika kisaikolojia na kupata tukio la ghafla lenye maumivu ndiyo inayotoa dira ya namna ya kumsaidia mtu wakati wa kumpatia msaada wa kitaalam.
3.     AINA ZA ATHARI ZA KISAIKOLOJIA
a)    Single traumatic experience;- katika aina hii, mtu anakuwa amekutana na tukio moja kwa mara ya kwanza. Mfano ameshuhudia mtu akiuawa.
b)    Multiple trauma;- Mtu anakuwa amekutana na matukio mengi ya kuumiza. Mfano mtu amepata ajali za gari mara kadhaa na kuvamiwa na watu wenye siraha.
c)     Continuous trauma;katika aina hii mtu anakuwa anaishi katika eneo ambalo kuna matukio ya kutisha na yanaendelea katika eneo hilo. Mfano nchi yenye mchafuko wa kisiasa wananchi wanaishi mazingira ya hatari kwa miaka mingi wakishuhudia matendo ya kikatili. Au askari ambae anafanya kazi katika mazingira hatarishi ya vita kwa muda mrefu.
d)    Complex trauma;- hii hutokea katikati ya watu wenye mahusiano maalum, kwa mfano ukatili wa kijinsia baina ya wana-ndoa, ndugu n.k.

4.     ATHARI ZA KAWAIDA ZA KISAIKOLOJIA

Baada ya mtu kuishi katika hali ya mawazo na maumivu yasiyopata utatuzi kwa muda mrefu, ndipo athari za kisaikolojia huanza kujitokeza “kuathirika kisaikolojia kunakufanya uvunjike moyo kwa ndani-kama nguo iliyochakaa’’. Zifuatazo ni baadhi za athari za kawaida za kisaukolojia;

                        i.         Mawazo ya kila wakati kuhusiana na tukio
                      ii.         Kuona, kusikia, au kuhisi harufu ambayo inafanana na tukio
                    iii.         Ndoto za usiku
                     iv.         Kukosa usingizi
                       v.         Kuanza kutumia dawa za kulevya
                     vi.         Kuongea kuhusu tukio lililokupata kila wakati
                   vii.         Mwili kuuma
                 viii.         Huzuni na kulialia
                     ix.         Kutaka kulipiza kisasi
                       x.         Hasira na sonona
                     xi.         Kuviepuka vitu vinavyoshabihiana na tukio
                   xii.         Kujiona hana thamani
                 xiii.         Kujitenga
                   xiv.         Kutomwamini yeyote.

Itaonekana ni ajabu, sio ya kawaida, ya kushanagaza na kushtua sana kuona mtu kama anakutana na tukio la kutisha halafu asionyeshe mwitikio wowote kati ya hizi zilizotajwa hapo juu.
Athari ikizidi kuwa kubwa zaidi  na ya kutisha na yenye maumivu, mtu kwa kawaida hujaribu kuonyesha mwitikio kati ya aina hizi mbili zifuatazo;
a)    Kuepuka;- mtu anajitahidi asikumbuke tukio lililompata, mahali pa tukio na kuepuka kitu chochote kinachoshabihiana na tukio. Mtu anajilinda kutokuongelea tukio na kuanza kutumia vileo au dawa ili kuzuia mawazo yanayomsumbua, na wakati mwingine tatizo likidumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi anapoteza uwezo wa kusikia na kuongea.

b)    Kujirudia;- Mara nyingi matukio ya kutisha huwa na tabia ya kujirudiarudia kwenye ufahamu wa mtu. Hii hutokea kwa njia ya kuwaza na kuota ndoto zinazohusiana na tukio. Jambo hujirudia kwenye akili ya mtu lakini mlengwa hataki, hivyo hujikuta anaingia kwenye mgongano wa mawazo  (hataki kuwaza lakini yanakuja). (approach avoidance conflict).


5.     ATHARI ZISIZO ZA KAWAIDA ZA KISIKOLOJIA
a.    Hallucinations (mareweruwe): kusikia, kuona au kuhisi vitu ambavyo kiuhalisia havipo.
b.    Delusions (dhana potofu): anang’ang’ania vitu ambavyo havina ukweli na kuvisimamia kwa gharama yoyote na wala huwezi kumuhamisha katika mawazo hayo.
c.     Severe depression: sonona iliyozidi
d.     Kuwa mchangamfu kupita kiasi, kuwa na matumizi makubwa ya fedha, kuwa na furaha kupita kiasi.
e.     Kuwa na matukio ya kutaka kujiua.

6.     MATOKEO YA ATHARI ZA KISAIKOLOJIA KWA FAMILIA NA MARAFIKI
-Matokeo ya athari hizi huwa zinaenda mbali zaidi ya mtu mwenyewe, kama kitu kibaya cha kuumiza kikitokea ndugu jamaa na marafiki pia huathirika. Hii ilithibitishwa na mama mmoja ambaye binti yake alibakwa, alionyesha hisia zake kwa kusema “Najua nimekuwa muoga sana juu ya binti yangu, hasa ninapokumbuka kuwa binti yangu amebakwa, nadhani mi naumia na nawaza zaidi kuliko yeye na matumaini yangu yote juu yake yamefifia”.

Mfano mwingine: mwanamke mmoja alikuwa akitoa maelezo juu ya hali iliyompata mume wake; “tangu amevamiwa na majambazi amebadilika sana, anakaa tu na hataki hata kuongea na mtu. Na wakati mwingine hutufokea bila sababu maalum, watoto wameshajifunza kukaa nae mbali kwa hofu”.

Mara nyingi watu walioumizwa kisaikolojia hujisikia vibaya wanapohisi kama familia au marafiki hawajalipokea vizuri jambo lake, hivyo huwafanya kuwa makini sana na watu wengine, na wakati mwingine huamua kuwaficha hata watu wa karibu sana juu ya mambo yanayowatokea kwa kuhofia wasije wakailetea huzuni familia.
Familia na marafiki hujisikia vibaya, wenye hasira na lawama nyingi juu ya aliyefanya ukatili dhidi ya ndugu yao.

7.     MATOKEO YA ATHARI ZA KISAIKOLOJIA KWA JAMII
-uwezekano wa mtu akipatwa na jambo baya, jamii nayo kuathirika na hali hiyo ni mkubwa.  Na jamii yetu mara nyingi inashindwa kutoa msaada kwa watu waliopatwa na matatizo kama ya kubakwa na aina nyingine nyingi za ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
Yafuatayo ni maelezo ya mtu aliyetendewa jambo la kikatili la kubakwa, na jamii badala ya kumtia moyo imekuwa ikimsema vibaya na kumtenga. Kwa maneno yake alisema: kitu kinachonisikitisha na kuniumiza moyo wangu ni namna jirani zangu, wanaofahamu yaliyonipata wanavyonitazama, Nimekuwa nikiwaona wananiteta na wamekuwa wakiniepuka”.
-matokeo ya kuumizwa kisaikolojia kwa jamii ya karibu, kama vile shule, makanisa na misikitini, lisichukuliwe kwa wepesi; watoto waelimishwe, na wazazi pia lazima wapate muda wa kuzungumzia mambo yahusuyo matukio magumu yaliyowapata kifamilia.
-wakati mwingine jamii yote huathirika na majanga ya asili kama vile; mafuriko, au vurugu za kisiasa ambazo hudumu kwa muda mrefu. Makundi haya pia yanahitaji unasihi wa karibu.

8.     MATOKEO YA ATHARI ZA KISAIKOLOJIA KWA WATOTO
·       kwa watoto wadogo huanza kunyonya vidole au kuongea kama katoto kachanga
·       wanakuwa na hasira na kujitupatupa chini au kugalagala.
·       Watoto wengi hujaribu kutaka kupata msaada kwa kujisingizia kuumwa; kichwa, tumbo, au mguu ili mradi asikilizwe.
·       Huepuka kwenda maeneo ambapo tukio lilimpata, na pia huepuka hata chakula ambacho alikula siku ya tukio au hukataa kuvaa nguo aliyovaa siku ya tukio.

Kuathirika kisaikolojia sio jambo la kujitakia, linaweza kumpata binadamu yeyote anayeishi katika dunia hii iliyojaa mambo mengi. Hivyo mara tu upatapo jambo gumu linalokosa majibu au utatuzi wa haraka, usisubiri mpaka ukose usingizi, ushindwe kula na watu kukuona umeshaanza kuwa sio wa kawaida. Tafuta msaada, kwani MAWAZI YAKO SIO MWISHO, TAFUTA MSAADA.

No comments:

Post a Comment