Ndizi na faida zake kiafya
Na
Zamda Haroun
Ndizi ni tunda muhimu Afrika Mashariki na katika nchi za
joto na hasa katika visiwa vya Caribbean. Mmea wake huitwa mgomba katika nchi
za Afrika Mashariki.
Tunda hili ambalo lina asili ya kusini mwa Asia huonekana na
rangi nzuri na mara nyingi tumezoea kuliona shambani au maeneo ya sokoni na
limeonekana kuwa na faida nyingi kiafya.
Miongoni mwa faida za tunda hili ni pamoja na kuboresha
ngozi, hususani maganda yake ambapo yanaaminika kusaidia kuimarisha ngozi pale
yanaposagwa vizuri na kuchanganywa na matunda mengine kama parachichi. Mchanganyiko
huo kwa pamoja husaidia kulainisha ngozi na kuifanya kuonekana vizuri na yenye
kung’aa.
Aidha, ndani ya ndizi kuna vitamin B6 na vitamini C, lakini
vitamini B6 ndio hupatikana kwa kiwango kikubwa zaidi ndani ya tunda hilo
kuliko vitamini C ambayo ni kidogo.
Hali kadhalika, ndizi husaidi kuongeza idadi ya chembe
chembe nyeupe za damu hivyo huweza kumsaidia mtu katika uboreshaji wa kinga
mwilini.
Faida nyingine za ndizi ni pamoja na kuongeza nguvu mwilini.
Hii ni kwa sababu tunda hilo huwa na sukari ijulikanayo kama ‘glucose,’ ambayo husaidia sana kuongeza
nguvu mwilini, ingawaje sukari hiyo huhitajika katika kiasi maalum mwilini.
Pamoja na hayo, ndizi pia huweza kusaidia sana kukukinga na kupata
vidonda vya tumbo kutokana na ‘compounds,’
mbalimbali zilizomo ndani ya tunda hilo. ‘Compounds,’
hizo ambazo hupatikana kwenye ndizi hujenga tabaka nene kwenye kuta za tumbo ambazo
husaidia tumbo kuzuia kuathirika na tindikali ijulikanayo kama ‘hydrochloric
acid’.
Aidha, ndizi zina ‘enzyme’
inayojulikana kama ‘protease inhibitor,’ ambayo
huzuia bakteria wasababishao vidonda vya tumbo.
Hizo ni baadhi ya faida chache tu za ndizi, ingawaje zipo nyingi
zaidi, lakini kwa leo tuhitimishie hapo. Hakikisha unadumisha kutumia tunda
hili mara kwa mara ili uweze kuimarisha afya yako zaidi.
No comments:
Post a Comment