Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Tuesday, December 16, 2014

Je, wajua madhara ya pombe kwa afya yako?

Na Seif Oddo
Pombe ni kinywaji ambacho hutumika kama kiburudisho miongoni mwa watu walio wengi duniani kote. Wengine hutumia pombe kwa lengo la kupunguza mawazo na wapo wanaotumia pombe kwa lengo la kuondoa aibu.


Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na uzalishaji wa pombe, zimekuwa zikijiingizia faida kubwa kutokana na bidhaa hizo kuwa na watumiaji wengi duniani kote.

Mbali na kuwa na wapenzi wengi, lakini utumiaji wa bidhaa hii kupita kiasi umekuwa ukileta madhara mbalimbali kwa watumiaji hawa kila kukicha.

Mashirika ya takwimu nchini Uingereza yanaripoti mnamo mwaka 2007, kulikuwa na vifo 8,724 ambavyo vilihusishwa na pombe nchini humo.

Nchini Scotland, shirika la NHS mnamo mwaka 2003 lilitoa makisio ya kwamba, kifo cha kila mtu mmoja kati ya vifo vya watu 20 vilitokana na pombe.

Utafiti uliofanyika mwaka 2009 pia uligundua ya kuwa watu 9,000 walikufa kutokana na magonjwa yaliyohusishwa na matumizi ya pombe.

Kituo cha udhibiti na uzuiaji wa magonjwa nchini Marekani kinaripoti kuwa, kutoka mwaka 2001 hadi kufikia mwaka 2005, kulikuwa na takribani vifo 79,000 vilivyotokana na matumizi ya pombe kupita kiasi.

Kiafya, matumizi ya pombe huleta madhara mbalimbali ndani ya mwili wa binadamu. 

Kwa mfano, ini huathirika vibaya kutokana na matumizi ya pombe kupindukia.

Pia tumbo nalo huathirika kutokana na kuchubuka kwa ngozi laini ya tumbo la chakula na kusababisha vidonda vya tumbo. Mbali na hapo, lakini pia ubongo nao huathirika, baadhi ya chembechembe za ubongo yaani ‘brain cells’ huharibika na kusababisha tatizo la kupoteza kumbukumbu.

Pia pombe huleta madhara katika moyo na mapafu ya binadamu. Kwa wanawake wajawazito, pombe huwasababishia kuharibika kwa mimba na hata kupelekea kujifungua mtoto mwenye mtindio wa ubongo.

Wataalam wa masuala ya afya wanaeleza kuwa, matumizi ya pombe kupita kiasi, husababisha matatizo ya mishipa, upungufu wa damu na matatizo ya kisaikolojia.

Wataalam hawa wanaeleza ya kwamba asilimia tisini ya watu wenye saratani ya tumbo ni watumiaji wa pombe kupita kiasi. Wanaeleza kuwa pombe husababisha ongezeko la mafuta ndani ya damu, lakini pia pombe huleta unene.

Pia pombe husababisha kutetemeka, kuzubaazubaa na hata kupauka kwa mwili.

Ndio maana hata katika vitabu vya baadhi ya dini kama vile dini ya Kiiislamu, pombe imeharamishwa kwa kuzingatia madhara yake kwa binadamu.

Mbali na madhara ya kiafya, pombe huleta mfarakano ndani ya jamii na hata huvuruga na kuondoa amani ndani ya familia. Pia pombe huathiri uchumi wa mtu kwani pombe ikishakuwa sugu ndani ya mwili wa binadamu (chronic), humfanya sehemu kubwa ya pato lake kuishia kwenye kununua pombe.

Ikumbukwe ya kwamba ndani ya pombe kuna kemikali ambazo huwa ni sumu katika mwili wa binadamu.

Inaelezwa ya kwamba pombe pia huleta madhara kama vile upungufu wa nguvu za kiume, kukosa hamu ya tendo la ndoa (loss of libido), kansa ya figo na kufanya figo kushindwa kufanya kazi yaani ‘renal failure’.

Pia pombe husababisha matatizo ya ganzi miguuni na mikononi ambayo kitaalam hujulikana kama ‘peripheral neuropathy’.

Lakini pia pombe huleta utapiamlo hasa kwa wale wanaokunywa sana huku lishe yao ikiwa duni na pia kuleta saratani ya umio yaani ‘oesophagus’.

Madhara ya pombe hayajaishia hapo lakini pia inaelezwa ya kwamba pombe husababisha saratani ya ini, kusinyaa kwa ini na hata saratani ya tumbo sambamba kabisa na vidonda vya tumbo.

Tazama maajabu haya, katika baadhi ya matangazo ya pombe mwishoni huelezwa kabisa kwamba ‘matumizi ya pombe kupita kiasi ni hatari kwa afya yako, tafadhali kunywa kistaarabu’.

Lakini watumiaji hawazingatii haya na hatimaye hunywa kwa kupitiliza na kujizolea matatizo mbalimbali. Epuka matumizi ya pombe kupindukia kwa ajili ya kulinda afya yako.

No comments:

Post a Comment