Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Friday, December 19, 2014

Presha na Tiba Yake

Na Juma Diwani
Ama kwa hakika unapozungumzia matatizo yanayowakabili watanzania wengi bila kujali rika hutoacha kuutaja ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu au kama lilivyozoeleaka katika masikio ya watanzania wengi ‘presha’.

Ugonjwa huu husababishwa na kuongezeka kwa msukumo wa damu katika kuta za mishipa ya damu, hali ambayo huufanya moyo kufanya kazi zaidi kuliko ilivyo kawaida ili kuweza kuzungusha damu mwilini. Kwa kawaida shinikizo la damu la mtu hupanda na kushuka kila siku, lakini baadhi ya watu hubakia juu na hapo ndipo mtu huweza kuambiwa anashinikizo la juu la damu.


Aidha, inaelezwa kuwa shinikizo la damu huweza kupelekea mifumo mingine ya mwili kuharibika, ambayo ni pamoja na figo kushindwa kufanya kazi vizuri, au mgonjwa kupatwa na maradhi ya kiharusi au shambulio la moyo.

Kwa kawaida shinikizo la damu ni muhimu kwa ajili ya kusukuma damu katika sehemu zote za mwili. Kiwango cha shinikizo la damu cha kawaida ni 120 mm Hg wakati moyo ukidunda (systolic)  na moyo unapokuwa umepumzika (diastolic) kiwango cha shinikizo la damu hupaswa kuwa 80 mmHg, hivyo inapoanza kuwa 130 mm Hg huweza kuwa ni tatizo.

Aina za tatizo la shinikizo la damu
Gazeti hili lilimtafuta Dk Emmanuel James, kutoka katika hospitali ya Tambuka reli, ilyopo wilaya ya Temeke, jijini Dar es salaam, ambaye alisema kuwa tatizo hili limegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni ‘primary hypertension’ na ‘secondary hypertension.’ Aina hii ya presha hii husababishwa na sababu za kimazingira kama msongo wa mawazo.

Dk Emmanuel, alisema kuwa aina hii ya ‘primary’ mara nyingi huwapata asilimia 90 hadi 95 ya watu wote wenye maradhi haya na huwa hakuna chanzo maalum cha kisayansi kinachofahamika vizuri.

Asilimia 5 hadi 10 ya ugonjwa wa shinikizo la juu damu husababishwa na shinikizo la damu aina ya pili, ambayo huitwa ‘secondary hypertension.’ Aina hii ya pili huhusihwa na sababu za kiafya kama mtu kusumbuliwa na magonjwa kama kisukari, matatizo ya moyo, figo kushindwa kufanya kazi nakadhalika.

Sababu zinazopelekea tatizo hili
Dk. Emamanuel alibainisha kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea kupata presha ni pamoja na msongo wa mawazo, ulaji wachumvi nyingi yenye madini ya Sodium, uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kupita kiasi, unene uliopitiliza, uhaba wa madini ya potassium, uhaba wa vitamin D pamoja na umri.

Daktari alieleza kuwa mfumo wa maisha kwa sasa umekuwa chanzo cha magonjwa mengi ukilinganisha na hapo awali..

“Sasa hivi hata familia yenye hali ya chini utakuta kama mboga ya majani baada ya kuipika chukuchuku atataka kuikaanga, siyo kama anakuwa amekula vitu vizuri sana hapana, lakini amekula vitu hatarishi,” alieleza Dk. Emmanuel.

Aidha, Mtaalam huyo alisema zamani watu walikuwa wanafanya shughuli nyingi sana na hivyo kuwa kama sehemu ya mazoezi, lakini sasa hivi hata watu wa hali ya chini pia hawajishughulishi sana na kusababisha tatizo hili kuwa kubwa zaidi.

Pia, Dk.Emmanuel aliongeza kwa kusema kwamba tatizo hili ni kubwa zaidi katika maeneo ya mijini kuliko vijijini huku akisema kuwa “ kijijini mtu akilima basi tayari amefanya mazoezi akichukua mihogo yake akichemsha kwake ni sawa, kwahiyo kwa kiasi kikubwa ni namna ya mtindo wa maisha.”

Dalili za tatizo hili
Presha ya kushuka
Dk. Emmanuel alifafanua kuwa miongoni mwa dalili ni pamoja na mapigo ya moyo kwenda taratibu,uchovu, maumivi ya kichwa, kizunguzu pamoja na misuli kuuma.

Presha ya kupanda
Daktari, alieleza kuwa, hakuna dalili za moja kwa moja za tatizo hili la presha, lakini mgonjwa huweza kuona dalili mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata maumivu ya kichwa hasa kwenye paji la uso na nyuma kwenye kisogo, pia mgonjwa huweza kuhisi kizunguzungu, kuchoka sana, ganzi katika mikono au miguu, kukojoa mara kwa mara  nyakati za usiku, mapigo ya moyo kwende mbio na inapokuwa kali sana mgonjwa huweza kupoteza fahamu.

Hata hivyo, alisema kuwa dalili hizo ni za awali na si wagonjwa wote huweza kupatwa na dalili hizo, na mara nyingine mgonjwa huweza kuwa na presha ya juu na asiwe na dalili hizo.

Watu walio katika hatari zaidi ya kupata presha
Dk Emmanuel alisema kuwa watu walio katika hatari zaidi ya ugonjwa huu ni wale ambao hawafanyi mazoezi, wenye unene uliokithiri, wavutaji wa sigara pamoja na wanywaji wa pombe, huku akiongeza kuwa sababu zote hizo huweza kudhibitiwa endapo mtu ataamu.

Pamoja na makundi ya watu hao kuwa katika hatari ya ugonjwa huo, Mtaalam huyo alifafanua kundi lingine ambalo lipo katika hatari ya ugonjwa huo ni watu wenye umri mkubwa (wazee.)

“Mtu unavyozeeka ule uwezo wa mishipa kutanuka na kusinyaa unapungua unakuwa unabana, kwahiyo kama damu ilibidi ipite kwenye bomba kubwa na sasa hivi limebana lazima itasukumwa kwa presha kubwa ili iweze kupita kwenye sehemu ambayo ni nyembamba.” alisema.

Kundi lingine lililo katika hatari ni wale wenye magonjwa ya kurithi (family history) na wale ambao wenye magonjwa ambayo huendana na presha hususani kisukari pamoja na watu weusi.

Ushauri kwa watanzania
Dk. Emmanuel alitoa wito kwa watanzania kujijengea hulka ya kufanya mazoezi mara kwa mara kwani hujenga afya ya mtu na kuwa na hulka ya kwenda kuaangali afya .

“Usisubiri hadi uanze kujisikia vibaya ndio uende hospitali badala yake tujiwekee taratibu za kupima afya zetu mara kwa mara, ugonjwa unapougundua katika hatua za awali husaidia kuweza kukabiliana nao kirahisi zaidi kuliko unapougundua kwa kuchelewa” alisema Dk Emmanuel.

Sambamba na hayo, aliwataka Watanzania kuweka mazoezi katika sehemu ya maisha yao ya kila siku kwani  ni dawa, huku akisisitiza kuzingatia kula vyakula katika mpangilio mzuri.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasemaje?
Ugonjwa wa shinikizo la damu la juu unakadiriwa kusababisha vifo vya watu milioni 7.5, ambayo ni sawa na asilimia 13 ya jumla ya vifo vyote duniani.
Aidha, taarifa zinasema kuwa kati ya watu wazima watatu duniani, mmoja huwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, hali ambayo husababisha karibu nusu ya vifo vyote kutokana na kiharusi na ugonjwa wa moyo.

Kwa upande wa Afrika WHO inaeleza kuwa zaidi ya asilimia 40 hadi 50 ya watu wazima wanakadiriwa kuwa na tatizo la shinikizo la damu na inaelezwa kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi.

Hata hivyo, taarifa zinasema idadi ya watu wenye shinikizo la damu usiodhibitiwa uliongezeka kutoka milioni 600 mwaka 1980 hadi kufikia bilioni 1 mwaka 2008.

Wataalam wa tiba asilia wanasemaje?
Akizungumza na gazeti hili mtaalam wa tiba asilia kutoka kituo cha Afya Bora Herbal Clinic, kilichopo kigogo, wilaya ya Ilala, jijini Dar es salaam, Dk. Mohamed Mkweli, alisema shinikizo la juu la damu (presha) ni ugonjwa unaosumbua watu wengi kwa sasa na tiba yake ya asilia ipo, ambayo huweza kumponya mgonjwa kabisa ndani ya mwezi mmoja hadi miwili bila ugonjwa huo kumrudia tena mhusika.

“Mgonjwa anapotumia dawa hii ya asili iitwayo ‘Faraja’ kutoka hapa Afya Bora Herbal Clinic mgonjwa hawezi kurudi kwangu tena kwa matibabu ya presha na wala kwenda hospitalini kwa tatizo hilo,” alilisisitiza Dk. Mkweli.

Aidha, Dk Mkweli alisema, ugonjwa huo umekuwa ukisumbua ulimwengu mzima na sababu kubwa ni watu kula vyakula vyenye mafuta mengi na mtindo wa maisha.

“Sasa hivi kila nyumba Tanzania na ulimwengu mzima wanakula vyakula vya mafuta na vyakula vya anasa ( vyakula mtumba) vya aina mbalimbali, hivyo kuwa katika hatari zaidi ya kupata magonjwa” alisema mtaalam huyo.

Pia alibainisha kuwa baadhi ya watu kutokana na ugonjwa huu kuharibu afya ya mtu taratibu na hatimaye kuangukia kupata magonjwa mengine kama kisukari na moyo ama kufa wameuita kuwa ni ‘silent killer’.


Halkadhalika aliwataka watanzania kuwa na hulka ya kufanya mazoezi kwa humfanya mtu kuwa na afya bora na kujikinga na magonjwa mbali mbali ikiwemo presha.

No comments:

Post a Comment