Wataalum
wa afya wanasema ugonjwa wa figo ni miongoni mwa magonjwa sugu duniani yanayoongoza
kwa vifo vingi na matibabu yake kuwa ni ya gharama hasa katika nchi
zinazoendelea kama Tanzania.
Ugonjwa
wa figo kushindwa kufanya kazi ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa utendaji kazi wa
kiungo hicho ambacho kazi yake kubwa ni kusafisha damu na kutoa maji machafu
yaliyozidi mwilini kupitia mkojo.
Hata hivyo,
wataalam wa afya wanatueleza kwamba ugonjwa wa figo unaweza kumuathiri mtu yeyote
wakati wowote bila ya kujali umri alionao.
Ili
kufahamu zaidi kuhusiana na ugonjwa huo, gazeti hili lilimtafuta Dk. Jacqueline
Shoo, daktari bingwa wa magonjwa ya figo kutoka kitengo cha figo cha Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, alisema kuwa pamoja na kwamba umri wa mtu umetajwa kuwa
ndiyo chanzo cha tatizo hilo, lakini umri siyo chanzo pekee kinachoathiri figo .
Alifafanua
kuwa vipo visababishi vya magonjwa mengine vinavyosababisha ugonjwa huo ikiwemo
shinikizo la damu la juu, kisukari na ugonjwa wa kuganda kwa mafuta kwenye
mishipa ya damu (lehemu). Hivi vyote kwa kiwango kikubwa husababisha maradhi
ya figo kushindwa kuafanya kazi.
Mtaalam huyo alisema kuwa, zipo
sababu kadhaa zinazosababisha maradhi ya figo za binadamu zikiwemo matumizi
mabaya ya dawa hasa za maumivu, dawa za kienyeji, baadhi ya dawa za Kichina,
uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, uzito na unene wa kupitiliza.
Dk. Shoo aliongeza, “tatizo la
ugonjwa wa figo linaongezeka kwa kasi kubwa hasa katika nchi zinazoondelea kama
Tanzania. Ili kugundua kama una tatizo hilo, unatakiwa kujiuliza maswali muhimu,
je, una shinikizo la damu, kisukari au mafuata kwenye damu?”
Mtaalam huyo pia alizitaja dalili
za ugonjwa huo kuwa ni kuvimba miguu na uso, kukosa au kupungua kiasi cha
mkojo, uchovu, kichefuchefu, kutapika, mkojo kugeuka kuwa na harufu mbaya ya
uvundo sambamba na kukosa hamu ya kula.
Dalili
zingine alisema ni mgonjwa kuwa na mwili dhaifu, mapigo ya moyo kwenda mbio,
kubanwa na misuli, kukojoa sana hasa wakati
wa usiku, mwili kuwasha, kupata michubuko kirahisi katika ngozi, upungufu wa
damu, kichwa
kuuma na kujihisi ganzi miguuni.
Dk. Shoo alifafanua pia, “ili kujikinga na tatizo hili ni
vizuri watu wakajenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara. Lingine ni watu
wajenge tabia ya kupenda kufanya mazoezi na kuepuka ulaji usiofaa hasa matumizi
ya chumvi na sukari kwa wingi, na kudhibiti kisukari na shinikizo la damu.”
Kwa mujibu wa Dk. Shoo, alisema
matibabu hutegemea na hatua mgonjwa aliyofikia kwani katika hatua 1 hadi 4
mgonjwa hupewa dawa na ushauri wa namna ya kujilinda na afya ya figo yake.
Mgonjwa anapofikia katika hatua
ya 5, maana yake yuko katika hali mbaya zaidi hivyo matibabu yake hutakiwa tiba
ya usafishaji wa figo na damu (renal dialysis). Daktari anasema kuwa tiba ya
usafishaji wa figo kwa kitaalam hemodialysis huhusisha utoaji wa maji yaliyojaa
mwilini, uchafu na pia sumu zitokanazo na vyakula au dawa. Dk. Shoo anasema
kuwa tiba ya ‘dialysis’ ni ya gharama kubwa kwa kuwa kila mgonjwa anapohitaji
kuipata, hutakiwa kutoa kiasi cha shilingi 300, 000 huku akitakiwa kuipata tiba
hiyo angalau mara tatu kwa wiki ambapo humgharimu shilingi 900,000 kila wiki.
“Hii huduma inafanyika hapa Muhimbili katika Kitengo cha Renal Dialysis Unit, na mgonjwa anatakiwa kuipata tiba hiyo maisha yake yote,” anasema Dk. Shoo.
Aliongeza kuwa dialysis ni mchakato wa kutoa maji yasiyohitajika kutoka kwenye damu kutokana na gharama kubwa ya matibabu pamoja na kukosekana kwa huduma ya kupandikiza figo nchini.
Aidha, alitoa wito
kwa Serikali na wadau kuendelea kutoa elimu ya ugonjwa huo kote nchini ili
kujenga uelewa wa kutosha kwa wananchi ili kukabiliana na namna ya kuweza kutunza
afya ya figo zao.
Wakati Tanzania ikiwa katika mchakato wa kuanza huduma ya upandikizaji wa figo mara ifikapo mwaka 2020, nchini Kenya katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta imeanza huduma ya upandikizaji figo tangu mwaka wa 1978 ikiwa hospitali pekee inayotoa huduma hiyo Afrika Mashariki.
Inaelezwa kuwa, tangu mwaka huo imepandikiza figo zaidi ya watu 99 na gharama zikiwa milioni 9 za Kitanzania, wakati huduma hiyo nchini India hugharimu shilingi milioni 26 hadi 33, za Kitanzania kwa mujibu wa mitandao. Takwimu za Chama cha
Figo Duniani zinaonesha kuwa mwanaume mmoja kati ya watano na mwanamke mmoja kati ya wanne walio katika umri wa miaka 65 hadi 74, huugua ugonjwa huo.
Kituo cha Utafiti wa Magonjwa Duniani (CDC) kinaeleza kuwa nchini Marekani inakadiriwa asilimia kumi ya watu wazima ambao ni milioni ishirini wanaugua ugonjwa wa figo
Gazeti hili pia lilimtafuta mtaalam wa tiba asilia Dk.
Karama Kiumbe, kutoka kituo cha Kiumbe Tradition Medcine Research, kilichopo
Mongolandege, Ukonga, jijini Dar es Salaam ambaye alisema kuwa tatizo hilo
limekuwa likiwasumbua watu wengi na wengine kwenda hadi nje ya nchi kutafuta
matibabu lakini kuna dawa ya asilia ambayo inaweza kutibu tatizo hilo.
Dk. Kiumbe alisema kuwa anayo dawa ambayo husaidia kuondoa
tatizo la figo ambayo inayoitwa ‘Sarmada’ ambayo hata kama mtu ana mawe
husaidia kuondoa.
“Ninayo dawa inayoitwa ‘Sarmada’ na hutibu figo kwa muda mchache
na hata kama kuna mawe huondoa kwa kipindi cha wiki moja mabadiliko
yanaonekana”
Serikali ifanye
jihada kuongeza madaktari kukabiliana na tatizo hili ambapo kwa sasa wapo
madaktari bingwa saba tu nchi nzima. Kwa aina ya ukubwa wa tatizo, bado madaktari
ni changamoto inayohitaji majibu katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya
afya figo duniani yaliyofanyika mwezi Mechi ambayo kauli mbiu yake ilikuwa ‘Figo
huzeeka kadiri mtu anavyozeeka. Jali afya ya figo zako.”
No comments:
Post a Comment