Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Thursday, October 2, 2014

Saratani ya ngozi inatibika



Na Kenneth Maganga na Juma Diwani

Saratani ya ngozi ni ugonjwa unaotokana na matokeo ya mgawanyiko wa seli za kwenye ngozi usio na mpangilio maalum, hivyo hupelekea kuunda uvimbe unaovamia na kuathiri viungo za mwili.

Saratani nyingi za ngozi huathiri seli kubwa mbili ambazo ni ‘squamous cells’ na ‘basal cells.’ Hivyo seli hizo zinapoathiriwa hupelekea mtu kupatwa na aina ya saratani iitwayo ‘Non-Melanoma Skin Cancer.’
Kuna aina zaidi ya 100 za saratani kwa kuzingatia ni kiungo gani cha mwili kimeathirika, lakini aina zote hizo huwa na sifa tatu zinazofanana ambazo ni ukuaji usiodhibitika wa seli, uwezo wa kuvamia na kushambulia ogani nyingine za mwili na uwezo wa kusambaa katika viungo vingine mwilini kupitia mishipa ya damu.

Aidha, aina hii ya saratani ya ngozi inaelezwa kusababishwa na mionzi ya jua iitwayo ‘ultraviolet rays’ ambayo kitaalam huitwa (UV-B) ambayo husababisha kuharibika kwa DNA au vinasaba mwilini.

Saratani huanza wakati sehemu mojawapo ya seli zinapoanza kukua pasipo udhibiti wowote na hivyo kusababisha ukuaji wa seli za saratani kutofautiana na ukuaji wa kawaida wa seli za mwili. Hali hiyo huchangia kuendelea kukua na kuzaa seli nyingine mpya zisizokuwa za kawaida na baadaye seli hizo za saratani huanza kushambulia ogani nyingine za mwili jambo ambalo halishuhudiwi katika seli za kawaida.

Makundi ambayo yapo katika hatari ya saratani hiyo
TABIBU lilizungumza na Dk. Yemela Ndibalema ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, ambaye alisema kuwa ugonjwa wa saratani huweza kumpata mtu wakati wowote wa maisha yake, lakini kuna makundi ambayo huweza kuwa katika hatari zaidi ya kupata saratani hiyo.

Makundi hayo ni pamoja na watu wenye upungufu wa kinga mwilini, wale ambao shughuli zao nyingi hufanyia katika maeneo yenye jua kwa muda mrefu nawalemavu wa ngozi (albino)
Wengine walio katika hatari ni wale wenye makovu makubwa hasa yatokanayo na kuungua, hali kadhalika na wenye magonjwa ya ngozi na ambao huzaliwa na uvimbe kwenye ngozi ambao baadaye huweza kubadilika na kuleta saratani.

Kwa mujibu wa utafiti wa Dk. Ndibalema uliofanyika mwaka huu na kutathimini wagonjwa waliofika katika taasisi hiyo ya magonjwa ya saratani nchini, alibaini kuwa kuanzia mwaka 2008 hadi 2011 asilimia 25 ya wagonjwa wote wa saratani aina ya ‘non-melanoma’ walikuwa ni walemavu wa ngozi yaani albino.

Inaelezwa kuwa watu wenye ngozi nyepesi mfano wazungu na wenye umri wa zaidi ya 60 ndio huwa katika hatari zaidi ya kupata saratani hii duniani kote.

Dalili za saratani ya ngoziDk. Ndibalema alisema kwamba miongoni mwa dalili za saratani hii ya ‘non-melanoma’ ni mgonjwa kuwa na kidonda ambacho hakiponi kwa muda mrefu (donda ndugu), na wakati mwingine kidonda hicho huweza kutokuwa na maumivu yoyote pia.

Aidha, daktari alisema vidonda hivyo mara nyingi hutokea sehemu za mwili ambazo huwa hazifunikwi hususani kichwani, shingoni na mabegani hii ni kwa sababu sehemu hizo zote hupatwa na mionzi ya jua.

“Hizo ndio sehemu kubwa ambazo vidonda huweza kutokea, ingawaje pia huweza kutokea sehemu nyingine tofauti na hizo,” alisema Dk. Ndibalema.
Pia daktari aliongeza kuwa mara nyingi kidonda cha mtu mwenye saratani kisipogundulika mapema na kupata matibabu sahihi huweza kuwa kikubwa na kusambaa hadi kufikia kwenye damu ambapo hatua hiyo inaelezwa kuwa ni hatari zaidi kwani huweza kusababisha kifo.

Hata hivyo, utafiti wa Dk. Ndibalema ulibainisha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wote waliotibiwa hospitalini hapo kuanzia mwaka 2008 hadi 2011 walikuwa na vidonda vikubwa vyenye zaidi ya sentimita 5.

Wagonjwa wengine 185 walionekana kuwa na vidonda vilivyochimbika sana kiasi cha kutokuwa na mgonjwa hata mmoja mwenye kidonda chenye chini ya sentimita 2 jambo ambalo ni hatari zaidi na husababisha matibabu kuwa magumu.
Shirika la Afya Duniani WHO wanasemaje?
Kwa mujibu wa WHO, wanasema watu milioni 3 hupata saratani kila mwaka, huku kati yao watu watatu ambao hupatikana na saratani mmojawapo huwa na saratani ya ngozi.

Inakadiriwa kuwa kila mwaka watu milioni 1.3 nchini Marekani hukabiliwa na saratani ya aina ya ‘non-melanoma,’ huku ikielezwa kuwa kati ya Wamarekani watano mmoja kati yao hupata saratani ya ngozi katika maisha yao.
Matibabu

Dk. Ndibalema alisema kuwa matibabu ya saratani hufanyika mara baada ya majibu ya vipimo kuthibitisha mgonjwa kuwa na saratani hiyo, huku yakitegemea na sehemu ambayo mgonjwa ameathirika.

Pia matibabu huzingatia hali ya mgonjwa, umri pamoja na mgonjwa anahitaji matibabu ya aina gani.

“Ni lazima mgonjwa apimwe magonjwa yote kabla ya kuchagua njia ya matibabu kwani unaweza kufanya matibabu ya upasuaji kumbe mgonjwa ana tatizo la kisukari, hivyo lazima ujue vitu vyote maana magonjwa mengine huweza kuathiri uponaji wa kidonda,” alisema daktari.

Hali kadhalika daktari alisema kuwa katika utafiti wake pia alibaini kwamba karibu asilimia 70 ya wagonjwa waliofika hospitalini hapo walikuwa na vidonda vikubwa, lakini walipona kabisa ndani ya miezi mitatu kwa kutumia njia ya tiba ya mionzi na kupitia tiba hiyo baadhi ya vidonda vilipungua kutoka sentimita 5 hadi sentimita 2.
Sambamba na hilo, daktari alisema kuwa wagonjwa ambao hufika hospitali mapema huwa na zaidi ya asilimia 95 ya kupata matibabu na kupona kabisa.

“Mgonjwa akija na kidonda chenye sentimita 2 au 3, uwezekano wa kupona huwa ni mkubwa, zaidi ya asilimia 95,”
alisema daktari.

Pamoja na hayo, daktari alisema saratani ya ngozi inatibika na mgonjwa anaweza kupona kabisa endapo atawahi kufika hospitalini na kupata matibabu sahihi.

Matibabu hayo, huhusisha ukataji wa sehemu iliyoathirika au matibabu ya mionzi na mara nyingine dawa maalum za kupaka ziitwazo ‘topico therapies’ hutumika endapo tatizo litaonekana si kubwa.
Jinsi ya kuepuka saratani hii
Daktari alishauri kuepuka kupatwa na jua hususani kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 10 jioni na endapo utashindwa kufanya hivyo alishauri kuvaa mavazi ambayo yatafunika mwili mzima au kupaka mafuta maalum yatayokukinga na mionzi ya jua (sun screen) na kufunika kichwa chako kwa kofia.


Mtu akipaka mafuta yanayoweza kukinga ngozi na miale hatari ya jua (sun screen)

Pia daktari alisema ni vizuri kuepuka kukaa kando kando ya maji, mchanga au zege hususani nyakati za kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 10 jioni kwani wakati huo huwa na miale ambayo si mizuri inayoweza kusababisha saratani.

“Hakikisha unajizuia kupatwa na jua kadri uwezavyo na kama kazi zako za kila siku zinahusisha mazingira ya jua basi ni vizuri ukajilinda,” alisema daktari.

Pia inaelezwa kuwa mtu anayejikinga na miale ya jua huwa na asilimia 99 ya kutopata saratani hii.

Mbali na njia hizo pia inaelezwa kuwa matumizi ya mafuta ya nazi, karanga na pamba huweza kusaidia ngozi iliyokwisha athirika na kuifanya kurejea katika hali ya awali, lakini pia imethibitika kuwa watu ambao hupendelea kunywa chai ya rangi mara kwa mara huwa na nafasi ndogo mno ya kupatwa na saratani ya ngozi.

Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) wanasemaje?
Kutokana na matumizi holela ya vipodozi kuelezwa kusababisha saratani ya ngozi TABIBU iliamua kumtafuta msemaji wa TFDA Gaudensia Simwanza kwa lengo la kufahamu wamefikia wapi katika kuthibiti vipodozi vyenye viambata sumu, ambapo alisema kuwa hadi sasa wameendelea kuhakikisha kuwa vipodozi vyenye viambata sumu haviingii nchini.
Vipodozi vingi vyenye viambata sumu husababisha kuharibu ngozi na kuifanya kuwa nyepesi na hivyo kusababisha miale hatari ya jua aina ya UV-B kupenya kirahisi kwenye ngozi na kusababisha saratani.

Hata hivyo, Simwanza alisema pamoja na jitihada hizo, lakini wamekuwa wakikabiliana na changamoto kubwa kwani watumiaji wa vipodozi hivyo wameendelea kutumia vipodozi hivyo pasipo kujali afya zao.

“Changamoto kubwa ni kwamba watumiaji vipodozi hivi bado hawajaacha kuvitumia na ndio maana vinaendelea kuingia sokoni kupitia njia za panya ila sisi tunaendelea kuhakikisha tunatoa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya vipodozi hivyo,” alisema Simwanza.

Simwanza aliongeza kuwa TFDA kwa sasa inatarajia kutoa elimu zaidi kuhusu matumizi ya vipodozi vilivyopigwa marufuku, huku wakilenga kuanza kueneza elimu hiyo katika shule za msingi na sekondari sambamba na vyuo vya elimu ya juu, huku lengo likiwa ni kuhakikisha watu wanaacha kutumia vipodozi vilivyopigwa marufuku.

Pamoja na hayo, Simwanza alisema kuwa “sasa hivi kuna kipodozi kingine kinaitwa ‘doro’ nacho ni kipodozi ambacho kina viambata ambavyo tunasema ni ‘hydroquinone’ ambacho huwa na madhara kwa mtumiaji.”

Sambamba na hayo, Simwanza ametoa wito kwa watumiaji wa vipodozi ambavyo havifai kuacha mara moja kwani madhara yake ni makubwa mno hususani kiafya.

“Kuna madhara ya kiafya, lakini pia kuna madhara ya kiuchumi maana baada ya kuzalisha utakuwa unaugua na kujitibia na hivyo kupoteza fedha nyingi ambazo ungefanyia maendeleo mengine ya kijamii,”
alisisitiza Simwanza.

Wataalam wa tiba asili wanasemaje?
Gazeti hili lilimtafuta mtaalam wa tiba asilia aliyejikita katika uchunguzi na uchambuzi wa mimea na tiba zake, kutoka Kituo cha Mazingira Natural Products, kilichopo mkoani Mbeya, Dk. Edger Kapagi, ambaye alisema kuwa watu wenye matatizo ya saratani wanaweza kula vyakula vya asili ambavyo vinaweza kupunguza athari ya tatizo hilo.

“Kuna baadhi ya vyakula mtu mwenye saratani anapokula huweza kupunguza athari au hatari ya kupata ugonjwa huo,” alisema Kapagi.

Aidha, Dk. Kapagi alifafanua kuwa vyakula amabvyo mtu anaweza kuvitumia ili kupunguza athari au hatari ya kupata kansa.

Alivitaja baadhi ya vyakula hivyo kuwa ni pamoja na mazabibu (grapes) ambapo aina hii ya matunda husaidia ngozi kupona haraka endapo imekwisha athirika na miale hatari ya jua.

Viazi vitamu na mboga mboga za njano, vyakula ambayo husaidia kupunguza hatari ya kupata saratani kutokana na kuwa na vitamin A, C na B6 pamoja na madini ya ‘potassium’ na nyuzi nyuzi (fiber.)

Mboga za kijani (dark green vegetables), huwa na vitamin E, A na E pamoja na madini ya ‘calcium,’ ‘magnesium,’ na ‘potassium’ ambayo husaidia kupunguza athari au hatari ya kupata saratani hii ya ngozi.

Korosho, parachichi na maharage pia ni miongoni mwa vyakula ambavyo husaidia kuboresha ngozi na hivyo kuifanya kuwa imara dhidi ya miale hatari ya jua ambayo husababisha saratani.

Vyakula vya nafaka kama ugali, wali na vingine vya aina hiyo huweza kupunguza athari au hatari ya kupata tatizo la kansa katika mwili wake.

Saratani ya ngozi inatibika, endapo mgonjwa atawahi kupatiwa matibabu, hivyo ni vizuri kuwahi kuonana na wataalam mara tu unapoona dalili za saratani ya ngozi kama zilivyoainishwa hapo awali.

Makala nyingine nyingi zitakazokuelimisha kuhusu afya yako utazipata kupitia gazeti lako la TABIBU linalopatikana mtaani kila siku ya Alhamis kwa shilingi 500/= tu.

No comments:

Post a Comment