Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Thursday, October 30, 2014

HABARI KUU ALHAMISI YA LEO 30/10/2014 KATIKA TABIBU

KIHARUSI KINATIBIKA

 Na Juma Diwani

Kiharusi au kwa jina la kitaalam ‘stroke’, ni mojawapo ya magonjwa yasiyoambukiza yanayotisha kwa binadamu. Ugonjwa huu huleta kupooza kwa viungo vya mwili vya binadamu na husababishwa na kuzibwa au kupasuka kwa mishipa inayopeleka damu katika ubongo na hatimaye seli za ubongo kufa kutokana na kukosa hewa ya oksijeni na lishe ya kawaida.

Kiharusi ni hali ya dharura ambayo hupelekea watu wengi kuwa nadhana ya uchawi wakati wanapatwa na tatizo hilo kwani linaweza kutokea mahala popote na wakati wowote.

Aina za Kiharusi 
Gazeti hili lilimtafuta Dk. Auson S. Rwehumbiza ambaye ni Mratibu wa Kisukari katika Kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza. Alisema kuwa tatizo hili linawasumbua watu wengi na zipo aina nyingi za kiharusi kulingana na wapi tatizo la kupooza hutokea. Rwehumbiza alifafanua miongoni mwa aina hizo kuwa ni:

1.    Kiharusi cha kukosa hewa kwenye ubongo (Ischemic stroke)
Aina hii ya kiharusi hutokea iwapo usambazaji wa damu katika sehemu ya ubongo hupungua na kusababisha tishu za ubongo za eneo lililoathirika kushindwa kufanya kazi zake vizuri.

Tatizo hili hutokea baada ya mshipa wa ateri kuziba kutokana na kuganda kwa damu, hali ambayo inasababisha damu isisafiri vyema na kuelekea kwenye ubongo.

2.    Kiharusi cha kuvuja damu ndani ya ubongo (Haemorrhagic stroke)
Aina hii ya kiharusi hutokea pale ambapo mishipa midogo ya damu ndani ya ubongo hupasuka na kusababisha kusambaa kwa damu ubongoni (cerebral hemorrhage). Mara nyingi aina hii ya kiharusi hutanguliwa na dalili za kichwa kuuma, au kuwepo kwa historia ya ajali ya kichwa.


Sababu zinazopeleka kiharusi
Kuna sababu nyingi zinazopelekea mtu kupatwa na ugonjwa wa kiharusi. Miongoni mwa sababu hizo ni;

      I.         Mishipa ya damu kuzungukwa na aina fulani za mafuta yasiyofaa mwilini, hali inayoitwa kitaalam kama ‘atherosclerotic plaque’ na hatimaye damu huganda katika mishipa.

    II.         Shinikizo la damu la muda mrefu lisilothibitiwa linaweza kusababisha kupasuka kwa mishipa midogo inayosambaza damu kwenye ubongo na hivyo damu kujaa kwenye ubongo.

 III.         Kuganda kwa chembechembe nyekundu za damu za mgojwa wa ‘sickle cell’ kunaweza pia kusababisha kuziba mishipa ya damu hivyo kusababisha kiharusi.

  IV.         Kutofanya mazoezi (mazoezi rafiki)

    V.         Kunywa pombe, uvutaji wa sigara na utumiaji wa madawa ya kulevya.

Dalili za kiharusi
Dk. Rwehumbiza alibainisha dalili zinazoweza kutumika kumtambua mtu anayesumbuliwa au anaelekea kupatwa na kiharusi, ambazo ni;
·      Kushindwa kutembea vizuri, hivyo kuathiri mwendo wake.
·      Kupungua kwa ufahamu wa hisia.
·      Kutokwa na mkojo bila kujijua.
·      Kupoteza uwezo wa kuongea, kusikia na kula au kunywa.
·      Ukosefu wa kumbukumbu
·      Madiliko ya upumuaji na kiwango cha moyo kudunda.
Tiba ya Kiharusi
Kwa mujibu wa Dk. Rwehumbiza, alisema kuwa miongoni mwa tiba ya kiharusi kwanza ni kutambua tatizo hilo limetokana na nini, kufanya mazoezi, kumeza ‘Junior aspirin’, kumeza virutubisho vya vitamini B pamoja na kuthibiti magonjwa sababishi kama kisukari na presha.
Angalizo: Usitumie dawa yoyote bila kupima na kufuata ushauri




Shirika la Afya Duniani linasemaje
Kila ifikapo tarehe 29 ya mwezi wa 10 kila mwaka, nchi zote huadhimisha Siku ya Kiharusi. Hata hivyo, shirika hilo linaeleza kuwa tatizo hili ni mojawapo ya magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo duniani.

Inakadiriwa kuwa watu zaidi ya milioni 5 duniani walifariki kutokana na kiharusi mwaka 2005 na asilimia 85 ya vifo hivyo vilitokea katika nchi zenye kipato kidogo na cha kati.
Watu walio katika hatari zaidi ya kupatwa na kiharusi
TABIBU lilimtafuta Dk. Herbert Mngoma kutoka katika Hospitali ya Hindu Mandal ambaye alifafanua juu ya watu waliokuwa katika hatari ya kupatwa na tatizo hilo. 

Alisema kuwa, watu walio na umri kuanzia miaka 40, wenye matatizo ya presha, kisukari na magonjwa ya moyo wapo katika hatari zaidi ya kupatwa na kiharusi.

Aliongeza kwa kusema kuwa watu walio na matatizo ya kisukari na presha na wakaacha kutumia dawa, nao wapo katika hatari zaidi ya kupatwa na kiharusi.

Vijana pia wapo katika hatari zaidi ya kupata kiharusi kutokana na tafiti zilizofanywa na ‘The Lancet Medical Journal’ za hivi karibuni. Tafiti hizi zilionesha kuwa zaidi ya watu 83,000 walio na umri wa miaka 20 na chini duniani wanapatwa na kiharusi.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa ifikapo mwaka 2030, vifo vinavyotokana na kiharusi vitakuwa mara mbili zaidi ya sasa.

Jinsi ya kuepukana na kiharusi
Dk. Mngoma alisema kuwa kuna njia mbali mbali za kuepukana na tatizo hilo linalowasumbua watu wengi.
·     Kwenda kupima afya zetu mara kwa mara
·      Kuwa na tabia ya kufanya mazoezi angalau kwa dakika 30 kila siku.
·      Kuacha kuvuta sigara
·      Kutumia chumvi na sukari kwa kiasi
·      Kutumia mafuta ya mimea
·      Kuthibiti kisukari

Hata hivyo, Dk.Mngoma ameiomba serikali itoe elimu ya kutosha kuhusu tatizo hilo kwani ni hatari na linawapata watu wengi kwa sababu nyingine zinazozuilika.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikitoa elimu ya kutosha kuhusu kiharusi kwa kina itawafikia watu wengi.”

Wataalam wa Tiba asilia wanasemaje
Gazeti hili lilimtafuta mtaalam wa tiba asilia Dk. Esibon N. Baroshigwa wa Amani Sanitarium Clinic iliyopo Dar es Salaam ambaye alisema kuwa watu wengi wanasumbuliwa na kiharusi kwa muda mrefu bila kupona lakini tatizo hili linatibika kwa njia mbadala.

Hata hivyo, Dk. Baroshigwa alisema kuwa miongoni mwa dawa zinazoweza kutibu tatizo hilo ni ‘Brain Activator’ na ‘OP’-Juisi ya matunda maalum ambazo zinapatikana katika kituo chake na mgonjwa anaweza kupona ndani ya mwezi mmoja.

Watu maarufu waliowahi kuugua kiharusi

Kwa mujibu wa mitandao mbalimbali, imeelezwa kuwa miongoni mwa watu waliowahi kuugua ugonjwa wa kiharusi ni pamoja Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999.

Kifo cha Mwalimu Nyerere kinasemekana kuwa hakikusababishwa na kiharusi bali kilitokana na ugonjwa wa saratani ya damu.

Wengine wanaosadikika kuugua ugonjwa huo ni pamoja msanii nguli wa maigizo, Said Ngamba maarufu kama ‘Mzee Small’ ambaye alifariki dunia mwaka huu.

Mwanasiasa maarufu aliyeishi nchini Urusi, Vladimir ‘Lenin’ Ilyich aliyefariki dunia mwaka 1924, alipatwa na kiharusi mara tatu maishani mwake. Matatizo yatokanayo na kiharusi ndiyo yaliyomuua. Rais wa 28 wa Marekani, Woodrow Wilson pia alifariki baada ya kuugua kiharusi cha ghafla. Wapo watu wengine wengi maarufu waliougua kiharusi ingawa alikuwa na ugonjwa wa saratani ya damu ambayo nayo huenda ilisababisha kifo chake.


Watanzania wanasemaje kuhusu tatizo hilo
TABIBU lilifanya mahojiano na Watanzania 20 ambao walisema kuwa kiharusi ni ugonjwa hatari unaowasumbua watu wengi na kuiomba Serikali kupitia wizara husika kutoa elimu ya kutosha kwa Watanzania.


No comments:

Post a Comment