Tabibu Tv

Tabibu Tv

TABIBU ADVERT

TABIBU ADVERT

GO WOMAN

GO WOMAN

GO MAN ADVERT

GO MAN ADVERT

tabibu new advert

tabibu new advert

EBOLA BBC NEWS

Saturday, October 11, 2014

UGONJWA WA FIGO UNATIBIKA


Mtoto anayesumbuliwa na tatizo la figo.


Na Kennedy Chaya, Dar
Wataalum wa afya wanasema ugonjwa wa figo ni miongoni mwa magonjwa sugu duniani yanayoongoza kwa vifo vingi na matibabu yake kuwa ni ya gharama hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Ugonjwa wa figo kushindwa kufanya kazi ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa utendaji kazi wa kiungo hicho ambacho kazi yake kubwa ni kusafisha damu na kutoa maji machafu yaliyozidi mwilini kupitia mkojo.

Hata hivyo, wataalam wa afya wanatueleza kwamba ugonjwa wa figo unaweza kumuathiri mtu yeyote wakati wowote bila ya kujali umri alionao.
Ili kufahamu zaidi kuhusiana na ugonjwa huo, gazeti hili lilimtafuta Dk. Jacqueline Shoo, daktari bingwa wa magonjwa ya figo kutoka kitengo cha figo cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema kuwa pamoja na kwamba umri wa mtu umetajwa kuwa ndiyo chanzo cha tatizo hilo, lakini umri siyo chanzo pekee kinachoathiri figo .

Alifafanua kuwa vipo visababishi vya magonjwa mengine vinavyosababisha ugonjwa huo ikiwemo shinikizo la damu la juu, kisukari na ugonjwa wa kuganda kwa mafuta kwenye mishipa ya damu (lehemu). Hivi vyote kwa kiwango kikubwa husababisha maradhi ya figo kushindwa kuafanya kazi.

Mtaalam huyo alisema kuwa, zipo sababu kadhaa zinazosababisha maradhi ya figo za binadamu zikiwemo matumizi mabaya ya dawa hasa za maumivu, dawa za kienyeji, baadhi ya dawa za Kichina, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, uzito na unene wa kupitiliza.

Dk. Shoo aliongeza, “tatizo la ugonjwa wa figo linaongezeka kwa kasi kubwa hasa katika nchi zinazoondelea kama Tanzania. Ili kugundua kama una tatizo hilo, unatakiwa kujiuliza maswali muhimu, je, una shinikizo la damu, kisukari au mafuata kwenye damu?”

Mtaalam huyo pia alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuvimba miguu na uso, kukosa au kupungua kiasi cha mkojo, uchovu, kichefuchefu, kutapika, mkojo kugeuka kuwa na harufu mbaya ya uvundo sambamba na kukosa hamu ya kula.

Dalili zingine alisema ni mgonjwa kuwa na mwili dhaifu, mapigo ya moyo kwenda mbio, kubanwa na misuli, kukojoa sana hasa wakati wa usiku, mwili kuwasha, kupata michubuko kirahisi katika ngozi, upungufu wa damu, kichwa kuuma na kujihisi ganzi miguuni.

Dk. Shoo alifafanua pia, “ili kujikinga na tatizo hili ni vizuri watu wakajenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara. Lingine ni watu wajenge tabia ya kupenda kufanya mazoezi na kuepuka ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi, na kudhibiti kisukari na shinikizo la damu.”

Kwa mujibu wa Dk. Shoo, alisema matibabu hutegemea na hatua mgonjwa aliyofikia kwani katika hatua 1 hadi 4 mgonjwa hupewa dawa na ushauri wa namna ya kujilinda na afya ya figo yake.

Mgonjwa anapofikia katika hatua ya 5, maana yake yuko katika hali mbaya zaidi hivyo matibabu yake hutakiwa tiba ya usafishaji wa figo na damu (renal dialysis). Daktari anasema kuwa tiba ya usafishaji wa figo kwa kitaalam hemodialysis huhusisha utoaji wa maji yaliyojaa mwilini, uchafu na pia sumu zitokanazo na vyakula au dawa. Dk. Shoo anasema kuwa tiba ya ‘dialysis’ ni ya gharama kubwa kwa kuwa kila mgonjwa anapohitaji kuipata, hutakiwa kutoa kiasi cha shilingi 300, 000 huku akitakiwa kuipata tiba hiyo angalau mara tatu kwa wiki ambapo humgharimu shilingi 900,000 kila wiki.

“Hii huduma inafanyika hapa Muhimbili katika Kitengo cha Renal Dialysis Unit, na mgonjwa anatakiwa kuipata tiba hiyo maisha yake yote,” anasema Dk. Shoo.

Aliongeza kuwa dialysis ni mchakato wa kutoa maji yasiyohitajika kutoka kwenye damu kutokana na gharama kubwa ya matibabu pamoja na kukosekana kwa huduma ya kupandikiza figo nchini.

Aidha, alitoa wito kwa Serikali na wadau kuendelea kutoa elimu ya ugonjwa huo kote nchini ili kujenga uelewa wa kutosha kwa wananchi ili kukabiliana na namna ya kuweza kutunza afya ya figo zao.

Wakati Tanzania ikiwa katika mchakato wa kuanza huduma ya upandikizaji wa figo mara ifikapo mwaka 2020, nchini Kenya katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta imeanza huduma ya upandikizaji figo tangu mwaka wa 1978 ikiwa hospitali pekee inayotoa huduma hiyo Afrika Mashariki.


Inaelezwa kuwa, tangu mwaka huo imepandikiza figo zaidi ya watu 99 na gharama zikiwa milioni 9 za Kitanzania, wakati huduma hiyo nchini India hugharimu shilingi milioni 26 hadi 33, za Kitanzania kwa mujibu wa mitandao. Takwimu za Chama cha 
Figo Duniani zinaonesha kuwa mwanaume mmoja kati ya watano na mwanamke mmoja kati ya wanne walio katika umri wa miaka 65 hadi 74, huugua ugonjwa huo.

Kituo cha Utafiti wa Magonjwa Duniani (CDC) kinaeleza kuwa nchini Marekani inakadiriwa asilimia kumi ya watu wazima ambao ni milioni ishirini wanaugua ugonjwa wa figo

Gazeti hili pia lilimtafuta mtaalam wa tiba asilia Dk. Karama Kiumbe, kutoka kituo cha Kiumbe Tradition Medcine Research, kilichopo Mongolandege, Ukonga, jijini Dar es Salaam ambaye alisema kuwa tatizo hilo limekuwa likiwasumbua watu wengi na wengine kwenda hadi nje ya nchi kutafuta matibabu lakini kuna dawa ya asilia ambayo inaweza kutibu tatizo hilo.

Dk. Kiumbe alisema kuwa anayo dawa ambayo husaidia kuondoa tatizo la figo ambayo inayoitwa ‘Sarmada’ ambayo hata kama mtu ana mawe husaidia kuondoa.

“Ninayo dawa inayoitwa ‘Sarmada’ na hutibu figo kwa muda mchache na hata kama kuna mawe huondoa kwa kipindi cha wiki moja mabadiliko yanaonekana”

Serikali ifanye jihada kuongeza madaktari kukabiliana na tatizo hili ambapo kwa sasa wapo madaktari bingwa saba tu nchi nzima. Kwa aina ya ukubwa wa tatizo, bado madaktari ni changamoto inayohitaji majibu katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya afya figo duniani yaliyofanyika mwezi Mechi ambayo kauli mbiu yake ilikuwa ‘Figo huzeeka kadiri mtu anavyozeeka. Jali afya ya figo zako.”


Thursday, October 9, 2014


Lile gazeti lako la pekee la Afya nchini Tanzania, Alhamisi ya leo tarehe 09/10/2014, lipo mtaani likiwa limesheheni habari lukuki, Makala, Hadithi za kusisimua na Katuni za kukuvunja mbavu na ukitaka kufahamu Maajabu ya Duniani pata nakala yako popote ulipo kwa gharama ya 500/= tu!

Na kwenye Michezo na Burudani Nisheedah


Thursday, October 2, 2014

Sidhani kama utakuwa sahihi endapo utaikosa kopi hii ya TABIBU!! Kwani limesheheni makala nyingi na nzuri zitakazokufanya usijutie thamani ya 500/= yako, hivyo hakikisha unaitafuta kopi hii mkoani kwako kwenye meza za wauza magazeti


 Michezo pia ni jadi yetu.......!

Saratani ya ngozi inatibika



Na Kenneth Maganga na Juma Diwani

Saratani ya ngozi ni ugonjwa unaotokana na matokeo ya mgawanyiko wa seli za kwenye ngozi usio na mpangilio maalum, hivyo hupelekea kuunda uvimbe unaovamia na kuathiri viungo za mwili.

Saratani nyingi za ngozi huathiri seli kubwa mbili ambazo ni ‘squamous cells’ na ‘basal cells.’ Hivyo seli hizo zinapoathiriwa hupelekea mtu kupatwa na aina ya saratani iitwayo ‘Non-Melanoma Skin Cancer.’
Kuna aina zaidi ya 100 za saratani kwa kuzingatia ni kiungo gani cha mwili kimeathirika, lakini aina zote hizo huwa na sifa tatu zinazofanana ambazo ni ukuaji usiodhibitika wa seli, uwezo wa kuvamia na kushambulia ogani nyingine za mwili na uwezo wa kusambaa katika viungo vingine mwilini kupitia mishipa ya damu.

Aidha, aina hii ya saratani ya ngozi inaelezwa kusababishwa na mionzi ya jua iitwayo ‘ultraviolet rays’ ambayo kitaalam huitwa (UV-B) ambayo husababisha kuharibika kwa DNA au vinasaba mwilini.

Saratani huanza wakati sehemu mojawapo ya seli zinapoanza kukua pasipo udhibiti wowote na hivyo kusababisha ukuaji wa seli za saratani kutofautiana na ukuaji wa kawaida wa seli za mwili. Hali hiyo huchangia kuendelea kukua na kuzaa seli nyingine mpya zisizokuwa za kawaida na baadaye seli hizo za saratani huanza kushambulia ogani nyingine za mwili jambo ambalo halishuhudiwi katika seli za kawaida.

Makundi ambayo yapo katika hatari ya saratani hiyo
TABIBU lilizungumza na Dk. Yemela Ndibalema ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, ambaye alisema kuwa ugonjwa wa saratani huweza kumpata mtu wakati wowote wa maisha yake, lakini kuna makundi ambayo huweza kuwa katika hatari zaidi ya kupata saratani hiyo.

Makundi hayo ni pamoja na watu wenye upungufu wa kinga mwilini, wale ambao shughuli zao nyingi hufanyia katika maeneo yenye jua kwa muda mrefu nawalemavu wa ngozi (albino)
Wengine walio katika hatari ni wale wenye makovu makubwa hasa yatokanayo na kuungua, hali kadhalika na wenye magonjwa ya ngozi na ambao huzaliwa na uvimbe kwenye ngozi ambao baadaye huweza kubadilika na kuleta saratani.

Kwa mujibu wa utafiti wa Dk. Ndibalema uliofanyika mwaka huu na kutathimini wagonjwa waliofika katika taasisi hiyo ya magonjwa ya saratani nchini, alibaini kuwa kuanzia mwaka 2008 hadi 2011 asilimia 25 ya wagonjwa wote wa saratani aina ya ‘non-melanoma’ walikuwa ni walemavu wa ngozi yaani albino.

Inaelezwa kuwa watu wenye ngozi nyepesi mfano wazungu na wenye umri wa zaidi ya 60 ndio huwa katika hatari zaidi ya kupata saratani hii duniani kote.

Dalili za saratani ya ngoziDk. Ndibalema alisema kwamba miongoni mwa dalili za saratani hii ya ‘non-melanoma’ ni mgonjwa kuwa na kidonda ambacho hakiponi kwa muda mrefu (donda ndugu), na wakati mwingine kidonda hicho huweza kutokuwa na maumivu yoyote pia.

Aidha, daktari alisema vidonda hivyo mara nyingi hutokea sehemu za mwili ambazo huwa hazifunikwi hususani kichwani, shingoni na mabegani hii ni kwa sababu sehemu hizo zote hupatwa na mionzi ya jua.

“Hizo ndio sehemu kubwa ambazo vidonda huweza kutokea, ingawaje pia huweza kutokea sehemu nyingine tofauti na hizo,” alisema Dk. Ndibalema.
Pia daktari aliongeza kuwa mara nyingi kidonda cha mtu mwenye saratani kisipogundulika mapema na kupata matibabu sahihi huweza kuwa kikubwa na kusambaa hadi kufikia kwenye damu ambapo hatua hiyo inaelezwa kuwa ni hatari zaidi kwani huweza kusababisha kifo.

Hata hivyo, utafiti wa Dk. Ndibalema ulibainisha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wote waliotibiwa hospitalini hapo kuanzia mwaka 2008 hadi 2011 walikuwa na vidonda vikubwa vyenye zaidi ya sentimita 5.

Wagonjwa wengine 185 walionekana kuwa na vidonda vilivyochimbika sana kiasi cha kutokuwa na mgonjwa hata mmoja mwenye kidonda chenye chini ya sentimita 2 jambo ambalo ni hatari zaidi na husababisha matibabu kuwa magumu.
Shirika la Afya Duniani WHO wanasemaje?
Kwa mujibu wa WHO, wanasema watu milioni 3 hupata saratani kila mwaka, huku kati yao watu watatu ambao hupatikana na saratani mmojawapo huwa na saratani ya ngozi.

Inakadiriwa kuwa kila mwaka watu milioni 1.3 nchini Marekani hukabiliwa na saratani ya aina ya ‘non-melanoma,’ huku ikielezwa kuwa kati ya Wamarekani watano mmoja kati yao hupata saratani ya ngozi katika maisha yao.
Matibabu

Dk. Ndibalema alisema kuwa matibabu ya saratani hufanyika mara baada ya majibu ya vipimo kuthibitisha mgonjwa kuwa na saratani hiyo, huku yakitegemea na sehemu ambayo mgonjwa ameathirika.

Pia matibabu huzingatia hali ya mgonjwa, umri pamoja na mgonjwa anahitaji matibabu ya aina gani.

“Ni lazima mgonjwa apimwe magonjwa yote kabla ya kuchagua njia ya matibabu kwani unaweza kufanya matibabu ya upasuaji kumbe mgonjwa ana tatizo la kisukari, hivyo lazima ujue vitu vyote maana magonjwa mengine huweza kuathiri uponaji wa kidonda,” alisema daktari.

Hali kadhalika daktari alisema kuwa katika utafiti wake pia alibaini kwamba karibu asilimia 70 ya wagonjwa waliofika hospitalini hapo walikuwa na vidonda vikubwa, lakini walipona kabisa ndani ya miezi mitatu kwa kutumia njia ya tiba ya mionzi na kupitia tiba hiyo baadhi ya vidonda vilipungua kutoka sentimita 5 hadi sentimita 2.
Sambamba na hilo, daktari alisema kuwa wagonjwa ambao hufika hospitali mapema huwa na zaidi ya asilimia 95 ya kupata matibabu na kupona kabisa.

“Mgonjwa akija na kidonda chenye sentimita 2 au 3, uwezekano wa kupona huwa ni mkubwa, zaidi ya asilimia 95,”
alisema daktari.

Pamoja na hayo, daktari alisema saratani ya ngozi inatibika na mgonjwa anaweza kupona kabisa endapo atawahi kufika hospitalini na kupata matibabu sahihi.

Matibabu hayo, huhusisha ukataji wa sehemu iliyoathirika au matibabu ya mionzi na mara nyingine dawa maalum za kupaka ziitwazo ‘topico therapies’ hutumika endapo tatizo litaonekana si kubwa.
Jinsi ya kuepuka saratani hii
Daktari alishauri kuepuka kupatwa na jua hususani kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 10 jioni na endapo utashindwa kufanya hivyo alishauri kuvaa mavazi ambayo yatafunika mwili mzima au kupaka mafuta maalum yatayokukinga na mionzi ya jua (sun screen) na kufunika kichwa chako kwa kofia.


Mtu akipaka mafuta yanayoweza kukinga ngozi na miale hatari ya jua (sun screen)

Pia daktari alisema ni vizuri kuepuka kukaa kando kando ya maji, mchanga au zege hususani nyakati za kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 10 jioni kwani wakati huo huwa na miale ambayo si mizuri inayoweza kusababisha saratani.

“Hakikisha unajizuia kupatwa na jua kadri uwezavyo na kama kazi zako za kila siku zinahusisha mazingira ya jua basi ni vizuri ukajilinda,” alisema daktari.

Pia inaelezwa kuwa mtu anayejikinga na miale ya jua huwa na asilimia 99 ya kutopata saratani hii.

Mbali na njia hizo pia inaelezwa kuwa matumizi ya mafuta ya nazi, karanga na pamba huweza kusaidia ngozi iliyokwisha athirika na kuifanya kurejea katika hali ya awali, lakini pia imethibitika kuwa watu ambao hupendelea kunywa chai ya rangi mara kwa mara huwa na nafasi ndogo mno ya kupatwa na saratani ya ngozi.

Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) wanasemaje?
Kutokana na matumizi holela ya vipodozi kuelezwa kusababisha saratani ya ngozi TABIBU iliamua kumtafuta msemaji wa TFDA Gaudensia Simwanza kwa lengo la kufahamu wamefikia wapi katika kuthibiti vipodozi vyenye viambata sumu, ambapo alisema kuwa hadi sasa wameendelea kuhakikisha kuwa vipodozi vyenye viambata sumu haviingii nchini.
Vipodozi vingi vyenye viambata sumu husababisha kuharibu ngozi na kuifanya kuwa nyepesi na hivyo kusababisha miale hatari ya jua aina ya UV-B kupenya kirahisi kwenye ngozi na kusababisha saratani.

Hata hivyo, Simwanza alisema pamoja na jitihada hizo, lakini wamekuwa wakikabiliana na changamoto kubwa kwani watumiaji wa vipodozi hivyo wameendelea kutumia vipodozi hivyo pasipo kujali afya zao.

“Changamoto kubwa ni kwamba watumiaji vipodozi hivi bado hawajaacha kuvitumia na ndio maana vinaendelea kuingia sokoni kupitia njia za panya ila sisi tunaendelea kuhakikisha tunatoa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya vipodozi hivyo,” alisema Simwanza.

Simwanza aliongeza kuwa TFDA kwa sasa inatarajia kutoa elimu zaidi kuhusu matumizi ya vipodozi vilivyopigwa marufuku, huku wakilenga kuanza kueneza elimu hiyo katika shule za msingi na sekondari sambamba na vyuo vya elimu ya juu, huku lengo likiwa ni kuhakikisha watu wanaacha kutumia vipodozi vilivyopigwa marufuku.

Pamoja na hayo, Simwanza alisema kuwa “sasa hivi kuna kipodozi kingine kinaitwa ‘doro’ nacho ni kipodozi ambacho kina viambata ambavyo tunasema ni ‘hydroquinone’ ambacho huwa na madhara kwa mtumiaji.”

Sambamba na hayo, Simwanza ametoa wito kwa watumiaji wa vipodozi ambavyo havifai kuacha mara moja kwani madhara yake ni makubwa mno hususani kiafya.

“Kuna madhara ya kiafya, lakini pia kuna madhara ya kiuchumi maana baada ya kuzalisha utakuwa unaugua na kujitibia na hivyo kupoteza fedha nyingi ambazo ungefanyia maendeleo mengine ya kijamii,”
alisisitiza Simwanza.

Wataalam wa tiba asili wanasemaje?
Gazeti hili lilimtafuta mtaalam wa tiba asilia aliyejikita katika uchunguzi na uchambuzi wa mimea na tiba zake, kutoka Kituo cha Mazingira Natural Products, kilichopo mkoani Mbeya, Dk. Edger Kapagi, ambaye alisema kuwa watu wenye matatizo ya saratani wanaweza kula vyakula vya asili ambavyo vinaweza kupunguza athari ya tatizo hilo.

“Kuna baadhi ya vyakula mtu mwenye saratani anapokula huweza kupunguza athari au hatari ya kupata ugonjwa huo,” alisema Kapagi.

Aidha, Dk. Kapagi alifafanua kuwa vyakula amabvyo mtu anaweza kuvitumia ili kupunguza athari au hatari ya kupata kansa.

Alivitaja baadhi ya vyakula hivyo kuwa ni pamoja na mazabibu (grapes) ambapo aina hii ya matunda husaidia ngozi kupona haraka endapo imekwisha athirika na miale hatari ya jua.

Viazi vitamu na mboga mboga za njano, vyakula ambayo husaidia kupunguza hatari ya kupata saratani kutokana na kuwa na vitamin A, C na B6 pamoja na madini ya ‘potassium’ na nyuzi nyuzi (fiber.)

Mboga za kijani (dark green vegetables), huwa na vitamin E, A na E pamoja na madini ya ‘calcium,’ ‘magnesium,’ na ‘potassium’ ambayo husaidia kupunguza athari au hatari ya kupata saratani hii ya ngozi.

Korosho, parachichi na maharage pia ni miongoni mwa vyakula ambavyo husaidia kuboresha ngozi na hivyo kuifanya kuwa imara dhidi ya miale hatari ya jua ambayo husababisha saratani.

Vyakula vya nafaka kama ugali, wali na vingine vya aina hiyo huweza kupunguza athari au hatari ya kupata tatizo la kansa katika mwili wake.

Saratani ya ngozi inatibika, endapo mgonjwa atawahi kupatiwa matibabu, hivyo ni vizuri kuwahi kuonana na wataalam mara tu unapoona dalili za saratani ya ngozi kama zilivyoainishwa hapo awali.

Makala nyingine nyingi zitakazokuelimisha kuhusu afya yako utazipata kupitia gazeti lako la TABIBU linalopatikana mtaani kila siku ya Alhamis kwa shilingi 500/= tu.

Mwarobaini hutibu magonjwa ya ngozi



Dk. Fadhili Emilly
Leo hii kupitia ukurasa wetu huu nimeona tufahamishane kuhusu faida za mti wa mwarobaini hasa katika suala zima la magonjwa ya ngozi yanayosumbua sana wanadamu.

Mwarobaini (Azadirachta indica) ni mti unaofahamika kwa uwezo wake wa kutibu magonjwa ya aina mbalimbali. Inaaminika kuwa mti huu asili yake ni nchini India na Burma. Mwarobaini hushamiri zaidi katika nchi za tropiki na una uwezo mkubwa wa kuhimili ukame.

Hapa nchini Tanzania, mti wa mwarobaini huweza kupatikana kwa urahisi kabisa katika maeneo mengi ya mijini na vijijini pia.

Jina hili la ‘mwarobaini’ linatokana na imani kuwa mti huu una uwezo wa kutibu magonjwa yapatayo arobaini, huku majani yake na mbegu zikitumiwa kama tiba kwa miaka mingi katika nchi mbalimbali duniani.

Kati ya magonjwa ambayo mti huu umetumika kutibu au kupoza ni pamoja na matatizo ya kusaga chakula tumboni, kisukari, saratani, magonjwa ya ngozi, malaria, ukungu (fungus), n.k.

Pia matawi ya mti huu hutumiwa kama mswaki na magome yake hutumiwa kama dawa ya kusafisha meno.

Hali kadhalika mafuta ya mbegu ya mwarobaini hutumika kutengenezea vipodozi na sabuni, lakini pia mbegu au mafuta yake hutumiwa kama dawa ya kuulia wadudu wanaoharibu mimea shambani.


Baada ya kufahamu baadhi ya faida mbalimbali za mti wa mwarobaini, leo nitakufundisha namna ya kutumia mti wa mwarobaini kujitibu magonjwa ya ngozi.

Mahitaji
Majani ya mti wa mwarobaini.
Sufuria
Mwiko
Jiko la gesi, mkaa au jiko la mafuta.

Hatua za kufuata

1. Chukua majani mabichi ya mti wa mwarobaini na uyaweke kwenye sufuria.

2. Chukua sufuria yako yenye majani ya mti wa mwarobaini na uiinjike kwenye jiko lenye moto wa wastani.

3. Chukua mwiko wako na uanze kuyakoroga majani yako taratibu hadi yakauke bila kuungua.

4. Majani yako yakishakauka, ipua sufuria yako, chukua majani yako yaliyokauka, yasage kisha hifadhi unga unga wako kwenye chombo cha plastiki.

Matumizi
Tumia vijiko viwili vya chai kwenye kikombe cha robo lita chenye maji ya moto, fanya hivyo mara mbili kwa siku kwa muda wa siku ishirini na moja.

Makala haya yameletwa kwenu na The Fadhaget Sanitarium Clinic, ambao hutoa huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa kutumia mimea asilia. Makao makuu yao ni Mbezi Beach Afrikana njia ya Salasala, Dar es Salaam. Au unaweza kuwasiliana nao kupitia namba; 0712 705 158, 0757 931 376, 0787 705 158, 0774 505 158. Pia unaweza kuwapata kupitia www.tv51.co.tz

Kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa kwa mwanaume



Na Dk. Emmanuel James

Tatizo la mwanaume kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa (hypoactive sexual desire disorder for men ) ni ile hali ya mwanaume kukosa msisimko na hamu ya kufanya tendo la ndoa.

Takwimu zinaonesha kwamba kila wanaume watano mmoja anakabiliwa na tatizo hili, huku tatizo hili likionekana kuwa ni chanzo kikubwa cha kujishusha thamani kwa baadhi ya wanaume na kukosa kujiamini.

Lakini pia tatizo hili limeonekana kuchangia msongo wa mawazo kwa wanaume wengi wanaosumbuliwa na tatizo hili.

Kukosa hamu ya kufanya mapenzi kunapelekea wanaume wenye tatizo hili kupunguza hata ukaribu na wenzi wao kwa kuogopa pengine mpenzi wake atagundua kuwa anatatizo hilo, hivyo wanaume wengi wenye tatizo hili hutumia sababu mbalimbali za uongo kwa wapenzi wao kwa lengo la kupunguza ukaribu nao.

Chanzo cha tatizo hili
  • Umri, kwa mwanaume anavyozidi kuongezeka kiumri hivyo hivyo pia hupunguza shahuku na hamu ya kushiriki tendo la ndoa.
  • Msongo wa mawazo (stress), kuwa na msongo wa mawazo unaotokana na migogoro ya kifamilia, mahusiano , hali ngumu ya kiuchumi au magonjwa yananyoathiri mfumo wa fahamu (mental disorder) yanaweza kuwa chanzo cha tatizo hili.
  • Matatizo ya kiafya (deseases), baadhi ya magonjwa huweza kumsababishia mwanaume kukosa hamu ya tendo la ndoa. Mfano wa magonjwa hayo ni pamoja na presha ya kupanda, mafuta menge mwilini, kisukari, UKIMWI n.k
  • Upungufu wa vichocheo vya hisia na hamu, (Hormonial Inbalance), kutolewa kwa kiwango kidogo cha kichocheo kijulikanacho kitaalam kama ‘testosterone’ ambacho huhusika na kuamsha hisia, msisimko na hamu ya kufanya mapenzi kwa mwanaume, hivyo pale kichocheo hicho kinapopungua kinaweza kuwa ni chanzo kikubwa cha tatizo hili na mara nyingine huweza kupelekea matatizo mengine kama asthma, kisukari n.k
  • Utumiaji wa baadhi ya madawa pia huweza kuwa chanzo cha tatizo hilo, hususani madawa yanayotumika kwa wagonjwa wa presha ya kupanda, kisukari, matatizo ya akili n.k. 
  • Upungufu wa “Dopamine” ambayo hutolewa na ubongo na kazi yake kubwa ni kumfanya mtu ajisikie vizuri pamoja na kuongeza hamu ya kushiriki tendo la ndoa. 
  • Uchovu pia ni miongoni mwa sababu za tatizo hili.
  • Unene kupita kiasi, kwa maana kwamba kadri unene unavyoongezeka huathiri uzalizaji wa ‘testosterone hormone,’ ambayo husaidia kuleta hamu ya kushiriki mapenzi.
  • Ulevi wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara na matumizi ya madawa ya kulevya kama kokeini, heroin nazo pia ni sababu za tatizo hili.


Matibabu 
Matibabu hutegemea na chanzo cha tatizo, lakini kwa ujumla utumiaji wa baadhi ya vyakula huweza kukusaidia kuongeza hamu ya kushiriki tendo la ndoa. Mfano wa vyakula hivyo ni pamoja na ndizi, parachichi, tikitimaji, zabibu, tangawizi, pilipili,pweza na ngisi hivyo ni baadhi ya vyakula vinavyoweza kusaidia kuondokana na tatizo hili.

Mwanaume mwenye tatizo hili huweza kukabiliwa na yafuatayo endapo hata pata matibabu ya maepema.

Msongo wa mawazo ambao utapelekea kusababisha matatizo mengine kama, presha ya kupanda, vidonda vya tumbo, n.k

Kushindwa kusimamisha uume.

Kushindwa kabisa kumridhisha mwenza wako na hatimaye kuvunja ndoa au uhusiano. 

Ushauri
Ni vizuri kuwahi mapema kuwaona wataalam mara tu unapohisi kuwa na tatizo hili, itakusaidia kupata utatuzi wa kina juu ya hili.

Kwa ushauri, vipimo pamoja na matibabu unaweza kutembelea kituoni kwetu Victoria Therapies kilichopo Mtoni Kijichi Manispaa ya Temeke. Au wasiliana nasi kupitia namba ya simu ifuatayo; 0658 027 027.

Thursday, September 25, 2014

Ebola: Liberia yatoa ya moyoni kwa Umoja wa Mataifa



Monrovia, Liberia

Hivi karibuni viongozi wa Liberia wameamua kujitokeza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuihakikishia taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa kuwa wameshindwa kuidhibiti homa ya Ebola, wakati ambapo Umoja huo umekuwa ukiahidi kuongeza juhudi za kimataifa ili kuzuia virusi hivyo.

Waziri wa Ulinzi wa Liberia, Brownie Samoukai, alitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuingilia kati, ili kuzuia ugonjwa huo wa Ebola, huku akisisitiza kuwa Ebola imekua ni tishio kwa usalama wa taifa hilo.

“Usalama wa Liberia uko hatarini kutokana na ugonjwa wa Ebola, ambao umekua ukisababisha vifo vya watu, na kuendelea kuenea katika maeneo mbalimbali ya nchi, ukiwemo mji mkuu wa Liberia, Monrovia”, alisema waziri Brownie Samoukai.

Mbali na hayo, Umoja wa Afrika AU umesema kuwa unatuma timu kadhaa za wataalam wa kutiba magharibi mwa Afrika kwa minajili ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa nchi ambazo zimeathirika zaidi na mlipuko wa homa ya Ebola zinahitaji zaidi uangalizi wa kitiba ili kuweza kukabiliana na janga hilo.

Umoja wa Afrika unataraji kutuma watu 100 ambao miongoni mwao watakuwemo madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wa huduma za kitiba ili kuunga mkono jitihada zinazotekelezwa sasa ili kuzuia kuenea kwa homa ya Ebola.

Homa hiyo ya Ebola inaonekana kuwa na nguvu zaidi tangu ilipogundulika mwaka 1976, na imekua vigumu kuidhibiti. Homa hiyo imesababisha vifo vya watu 2296 huku watu 4293 wakiwa wameambukizwa virusi vya Ebola. Nchini Liberia pekee watu 1224 wamefariki kutokana na ugonjwa huo wa Ebola, Shirika la Afya Duniani WHO, limethibitisha.

Pamoja na nchi hizo kuonekana kuathirika zaidi, lakini pia vifo vya watu saba vimeorodheshwa kutokea nchini Nigeria ikiwa ni taifa linalostawi kiuchumi barani Afrika

Sambamba na hayo, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo, ambako kunaripotiwa aina nyingine ya Homa ya Ebola tofauti na ile inayoshuhudiwa Afrika ya magharibi. imeordhesha vifo vya watu 32 ambao wamefariki kutokana na Homa hiyo.