Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Thursday, September 11, 2014

WHO: Tanzania inashika namba mbili kwa kujinyonga



Shirika la afya Duniani (WHO) hivi karibuni limetoa ripoti yake inayoainisha idadi ya watu wanaojiua duniani, huku hali ikionesha kuongezeka na kufikia kiwango cha kutisha zaidi, ambapo katika ripoti hiyo Tanzania imeonekana kushika nafasi ya mbili barani Afrika. 
 
Ripoti hiyo ilieleza kwamba Tanzania iko katika nafasi hiyo ya pili barani Afrika ikiwa na asilimia 24.9 ya vifo hivyo vya kukusudia.

Hata hivyo, Shirika hili limesema kuwa katika kila sekunde 40 mtu mmoja anajiua na hivyo kusema kuwa tatizo hilo ni la kiafya pia na linahitajika kushughulikiwa.

Utafiti huo uliohusisha nchi 172 duniani ulizitaja nchi za barani Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu wanaojiua, ambapo nchi hizo ni pamoja na Msumbiji, Tanzania, Burundi, Sudan Kusini na Uganda. Na D.W

Wednesday, September 3, 2014

HUU NDIO MUONEKANO WA UKURASA WA MICHEZO NDANI YA GAZETI LA TABIBU ALHAMISI HII SEPTEMBA 04


HUU NDIO MUONEKANO WA GAZETI LAKO LA TABIBU WIKI HII SEPTEMBA 4, HAKIKISHA HUKOSI NAKALA HII.


Njia za kuepuka virusi hatari vya Ebola



Ebola ni mojawapo ya virusi hatari zaidi ulimwenguni, lakini ugonjwa huu hauambukizwi kupitia hewa, hivyo basi huwezi kuambukizwa ebola kama homa ya kawaida.

Madaktari wanasema kuepuka Ebola ni rahisi sana iwapo mtu atafuata tahadhari hizi muhimu zaidi:

1. Nawa mikono kwa sabuni na maji
Nawa mikono kila baada ya shughuli yoyote, hakikisha unatumia sabuni na maji safi na utumie taulo kujikausha. Ingawaje jambo hili linaweza kuwa gumu kwa wanaoishi kwenye makazi duni, na walio vijijini ambako maji safi hayapatikani kirahisi, lakini ni mbinu iliyothibitishwa kuweza kuua virusi vya ebola.


Pia wataalam wanashauri kusalimiana kwa mikono kuepukwa kwa ujumla.
Dk Unnis Krishnan wa Plan International aliarifu BBC, kuwa ebola husambazwa haraka watu wanapowasiliana ana kwa ana na maji maji ya kimwili ya waliougua. Hivyo ni vizuri kutumia njia nyingine za kujuliana hali.

2. Hakuna kugusana
Iwapo unashuku kuwa mtu ana ebola, usimguse. Ingawaje inaweza kuonekana kuwa si maadili mema unapoona unaowapenda wakihisi uchungu na unataka kuwakumbatia na kuwahudumia, lakini haiwezekani.

3. Epuka miili ya wafu
Iwapo unadhani mtu amefariki baada ya kuugua ebola, usiguse mwili wao, hata kama ni mila au desturi ya maziko. Hii ni hatari kwa sababu baada ya mtu anapofariki bado huweza kuambukizwa ebola kutoka kwa miili yao kwani bado inatoa maji maji ya mwili, ambayo huweza kuwa hatari zaidi.Ni vyema kufanya mipango ya kupata timu ya magwiji kushughulikia mwili huo haraka iwezekanavyo kwani ni hatari kuacha mwili wa mfu kwa muda mrefu katika eneo la makazi.


4. Usile nyama ya porini
Epuka kuwinda, kugusa, au kula nyama ya porini, kwa mfano popo, nyani na sokwe, kwani wanasayansi wanaamini kuwa hiyo ndiyo chanzo cha maambukizi kwa binadamu.



Pia wataalam wanashauri hata kama mnyama fulani wa porini huliwa katika eneo lenu na nyama yake ni tamu ni vyema kuepuka myama huyo kwani nyama yake au damu huweza kuwa na virusi hivyo. Hakikisha vyakula vyote vinapikwa inavyostahili.

5. Usiwe na hofu
Kueneza uvumi huongeza hofu. Usiogope wafanyakazi wa huduma za afya, pia usiamini matibabu ya kiasili ambayo hayajathibitishwa kutoa afueni, kwani suala hilo limechangia sana ongezeko la kuenea kwa virusi vya Ebola katika nchi zilizoathirika.
Mtu huweza kupata maambukizi ya ugonjwa huu endapo utagusa maji maji ya kimwili- mkojo na kinyesi, matapishi, kamasi, mate, machozi, na mbegu za kiume na majimaji ya uke- vyote huweza kueneza ebola endapo mhusika atakuwa ameathirika na ugonjwa huo.


Dalili za mtu aliyeugua ni joto mwilini, maumivu ya misuli na viungo, vidonda kooni, kuumwa na kichwa, na uchovu, kufuatiwa na kichefuchefu, kutapika na kuharisha, ambapo mtu huweza kutoa damu pia. Ebola bado haina tiba sasa. Na BBC

Tambua umuhimu wa tende kwa afya yako



Na Seif Oddo
Tende ni tunda ambalo limethibitishwa kuwa na manufaa makubwa katika mwili wa binadamu endapo litatumika ipasavyo.

Tunda hili ni maarufu katika nchi za mashariki ya kati na sehemu nyingine duniani. Lakini asili ya tunda hili ni kutoka katika nchi za kiarabu na liliingia Afrika Mashariki mnamo karne ya 7.

Nchini Tanzania tende hupatikata kwa wingi kisiwani Zanzibar pamoja na Pemba, ambapo imekua kama ni sehemu ya chakula cha kiutamaduni visiwani humo. Mbali na ladha yake nzuri ya tenda, lakini pia tunda hili limekuwa likitajwa hasa katika vitabu vitukufu vya dini.

Aidha, tunda hili limekuwa likitumiwa sana na waumini wa dini ya Kiislamu hususani katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Ambapo Shekhe Khalfan Tiwany wa Chakechake Pemba anaeleza kuwa, tende ni miongoni mwa vyakula vilivyotajwa katika Quraan Tukufu. Huku akiongeza kuwa, katika kisa maarufu cha kuzaliwa Nabii Issa, mama yake Bi. Maryam aliamriwa kula tende baada ya kujifungua, ili kurudisha damu nyingi aliyoipoteza baada ya kujifungua pamoja na kurudisha nguvu ya mwili wake kwa haraka.

Mbali na hayo, wataalam wa tiba wamethibitisha kuwa tende ni chanzo cha virutubisho na nishati mwilini, pia huwezesha kuupatia nguvu mwili kwa haraka sana na hii ndio sababu ya tunda hili kutumika kwa wingi katika Mfungo wa Ramadhani, kwani waumini waliofunga hulitumia tunda hili ili kurudisha nguvu na nishati iliyopotea mchana kutwa walipokuwa wamefunga.


Wataalam wanaendelea kueleza kwamba, ndani ya tende kuna virutubisho kama vile ‘calories,’ ‘calcium,’protein,’ ‘potassium,’ ‘magnessium,’phosphorous,’vitamin A’foliate’ na ‘carbohydrates,’ ambavyo vyote ni muhimu katika miili yetu kiafya.

Hata hivyo, Dk, Ally Khamis wa Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja Kisiwani Zanzibar ameeleza kuwa, tende ni chakula cha afya na huwa na mkusanyiko wa ‘vitamin A,’ ambayo husaidia katika kuongeza nuru ya macho, pia kuna madini ya ‘calcium,’ ambayo husaidia kuimarisha mifupa, hali kadhalika ndani ya tunda kuna ‘vitamin B6’ na B12, ambazo husaidia katika usagaji na ufyonzaji mzuri wa chakula na kuingia katika mishipa ya damu.

Hali kadhalika, tunda hili linaelezwa kuwa na uwezo wa kutoa kinga dhidi ya maradhi ya saratani ya tumbo (Colon Cancer). Pia huweza kuimarisha moyo na kuukinga dhidi ya maradhi.

Mbali na hayo, tende pia hutibu maradhi ya tumbo kama vile kujaa gesi, kuharisha na kuchafuka kwa tumbo. Pia wataalam wanaeleza kuwa tende husaidia kuondoa sumu mwilini na kusaidia kuongeza nguvu za kiume endapo litatumika kwa kufuata ushauri wa kitabibu.

Tende ni tunda pekee lenye uwezo wa kuupa mwili vitu vinne kwa wakati mmoja ambavyo ni protini, wanga, vitamin na mafuta. Pia tende ni tunda ambalo huyeyuka haraka sana tumboni, hivyo kutolipatia tumbo shida ya kufanya umeng’enyaji (Digestion).

Sambamba na hayo, wataalam wa afya wanaeleza kuwa, tunda hili husaidia kutanua misuli ya mji wa mimba na hivyo basi humsaidia mwanamke kutopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua. Aidha, wataalam wa afya wanaendelea kueleza kwamba tende ni chakula bora kwa wanawake wanaonyonyesha kutokana na kusaidia kuyapa maziwa virutubisho muhimu ambavyo humfanya mtoto kuwa na afya bora.

Mbali na hayo, tende ni chanzo kizuri cha madini ya chuma, ambayo husaidia kuwapa ahueni watu wenye upungufu wa damu mwilini. Hivyo basi mbali na kupenda kutumia tende kipindi cha Mwezi wa Ramadhani tu, ni vizuri tukatumia siku zote kama tunavyotumia vyakula vingine, ili kuweza kuimarisha afya zetu kikamilifu.

Makala kama hizi hupatika katika gazeti la TABIBU ambalo linatoka kila siku ya Alhamis na kupatikana nchi nzima kwa shilingi 500/=


Mtindi husaidia kutibu shinikizo la damu


Mtindi unaorodheshwa kuwa ni miongoni mwa vyakula bora kutokana na kuwa na virutubisho vingi  vya aina mbalimbali ambavyo vina faida nyingi katika mwili wa mwanadamu .

Miongoni mwa virutubisho vinavyopatikana katika maziwa ya mgando (mtindi) ni pamoja na calcium, phosphorus, rhiboflavin (vitamin B12), potassium, iodine na vinginevyo.

Asilimia kubwa ya wanajamii wengi hupendelea kusindika kinywaji hiki kwa muda mrefu na kisha kukitumia, hususani jamii ya Wamasai na Kimang’ati, ambao huyaweka maziwa hayo kwenye kibuyu.

Mbali na kuwa virutubisho hivyo vinapatikana ndani ya maziwa ya mgando ambayo wengi tunayafahamu kama mtindi, pia hupatikana bakteria hai ambao ni muhimu kiafya katika mwili wa binadamu (probiotics).


Watafiti wamebaini kuwa bakteria wanaopatikana katika mtindi hurefusha maisha kwa wazee, ni kinga kubwa kwa kina mama kutokana na maambukizo ya magonjwa ya ukeni na hata hupelekea  kupunguza  kiwango kikubwa cha shinikizo la damu la juu (high blood pressure level), lakini pia husaidia  kupunguza uzito mkubwa na unene uliopitiliza.

Kama inavyojulikana, kiwango cha shinikizo la damu kikiwa juu huleta magonjwa kama mshtuko wa moyo na kiharusi. Tafiti hizo zinasema kuwa probiotics zinasaidia kudhibiti viwango vya insulin, lehemu  na glukosi mwilini visizidi.

Wataalam hao kupitia tafiti hizo wamesema kuwa  maziwa yamgando (mtindi) yameokoa maisha ya walio wengi baada ya tathimini kutoka kwa wagonjwa zaidi ya 540 waliosumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu.

Pamoja na hayo, idadi kubwa ya wagonjwa waliotumia kinywaji hiki walifanikiwa kupona baada ya muda usiopungua wiki nane, hivyo inapendekezwa kutumia kinywaji hiki kama sehemu ya lishe yetu.


Makala nyingine nyingi nzuri zitakazokuelimisha kuhusu afya ya tiba za asili hupatikana kila siku ya Alhamis ndani ya gazeti la TABIBU kwa shilingi 500/= tu. Hakikisha hukosi nakala yako.