Tabibu Tv

Tabibu Tv

EBOLA BBC NEWS

Tuesday, August 12, 2014

JE UNAFAHAMU MBOGA ZA MAJANI NA MATUNDA HUWEZA KUOKOA MAISHA YAKO




Na, Asha Habibu, Kwa msaada wa mtandao

Watafiti nchini Uingereza wanasema kula matunda na mboga za majani mara saba kwa siku inakuwezesha kuwa na afya zaidi kuliko mara tano iliyokuwa imependekezwa hapo awali na shirika la afya duniani

Utafiti huu mpya unasema kuwa kula matunda mara saba kwa siku kunaweza kuokoa maisha yako kutokana na vifo vya mapema.

Utafiti uliofanyiwa wanaume na wanawake, 65,226, ulionyesha kuwa matunda mengi aliyokula mtu mmoja yalimpunguzia uwezo wa kufariki katika umri wowote.

Aidha, utafiti huo unabainisha kuwa ikiwa utakula matunda mara saba kwa wiki uwezo wako wa kupatwa na magonjwa yanayotishia maisha yako, unapungua kwa asilimia 42.

Wataalamu wanasema kuwa mifumo mingine ya maisha kama vile kutovuta sigara na kutokunywa pombe kupindukia pia imechangia kupungua kwa vifo.

Hata hivyo, watafiti hao walisema kuwa hawakuzingatia tu faida za matunda na mboga bali mambo mengine mengi.

Watafiti katika Chuo kikuu cha University College London, walitathmini data iliyokusanywa kati ya mwaka 2001 na 2008, iliyowapa mweleko kuhusu afya ya watu wanaokula matunda kwa wingi.

Utafiti huo ulitathmini idadi ya vifo kwa ujumla pamoja na vifo vinavyotokana na Saratani, maradhi ya Moyo na Kiharusi na kugundua kuwa vifo vya mapema vilipungua kulingana na mtu anavyokula matunda na mboga za majani.

Mboga za majani ndizo zilikuwa na uwezo mkubwa wa kulinda mwili dhidi ya maradhi hata zaidi ya matunda.

Hata hivyo, maji ya matunda hayakuwa na manufaa makubwa huku matunda yanayopakiwa kwenye mikebe yakionekana kuongeza tisho la kifo.

Wataalamu wanasema kuwa wangali wanaendelea na utafiti wao na kwamba kuna mambo mengine mengi yanayochangia afya ya mtu.

Kwa habari nyingi zaidi usikose kupata nakala yako ya gazeti la Afya TABIBU kila Alhamisi kwa shilingi 500/= tu.

Sunday, August 10, 2014

Imarisha afya yako kwa kufanya mazoezi






Na Seif K. Oddo
 Ni ukweli usiopingika, japokuwa tuliowengi hatufahamu ya kwamba magonjwa mengi yanayosumbua miili yetu tunajitengenezea au kujisababishia sisi wenyewe. Miili yetu imeumbwa ili iweze kutumika katika kiwango fulani, hivyo kuitumia chini au juu ya kiwango hicho husababisha magonjwa mbalimbali.
Maendeleo ya teknolojia yameleta starehe au raha na kurahisisha maisha kwa kiasi kikubwa, ila nyuma ya maendeleo haya ya teknolojia yamebeba athari za kiafya katika miili yetu bila ya sisi kufahamu. Kwa mfano watu wengi kwa sasa wamekuwa wakipenda kutumia magari katika matembezi, tena hata kwa umbali mdogo, watu wengi hupenda kuketi kwa muda mrefu majumbani wakiangalia tamthilia katika televisheni zao. Walio wengi wanapenda kufanya kazi zisizotumia nguvu hata kidogo, pia watu wengi hupenda kutumia lifti kupanda katika majengo marefu wanapokwenda maofisini mwao.
 Mfumo huu wa maisha ya aina hii ndio hasa unaopelekea tushindwe kutumia miili yetu ipasavyo pamoja na virutubisho tunavyokula katika vyakula mbalimbali. Miili yetu haihitaji kiasi kikubwa cha virutubishi hivi na visipopunguzwa hurundikana na kuwa sumu ambayo husababisha magonjwa mbalimbali kama vile kisukari, saratani na magonjwa mengineyo.
Hapo ndipo umuhimu wa kufanya mazoezi unapochukua nafasi kubwa katika kulinda na kuimarisha afya ya binadamu. Mazoezi ni tiba na pia ni kinga ya mwili wa binadamu dhidi ya magonjwa mbalimbali.Kupitia mazoezi, tunaweza kupunguza mafuta na kuondoa baadhi ya sumu ndani ya miili yetu na hata kupunguza uzito wa mwili ambao pia huwa ni kikwazo kiafya.
Hivyo basi tunashauriwa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya za miili yetu. Ni vyema mtu akatenga muda maalum kwa ajili ya kufanya mazoezi, kama unavyotenga muda maalum kwa ajili ya kula. Inashauriwa mbali na kutenga muda huu, pia ni lazima kuheshimu kwa kufuata ratiba ya mazoezi uliojipangia ili kufikia lengo. Kuna baadhi ya sehemu za miili yetu hazitibiki kwa dawa au kwa upasuaji isipokuwa kwa mazoezi pekee. Hivyo basi mazoezi ni kitu muhimu sana kuliko watu wengi wanavyodhani.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, imebainika kuwa kwa kufanya mazoezi unawezesha mwili kutumia virutubisho ipasavyo, kwani hakutokuwa na kinachohifadhiwa ama kubaki mwilini kinyume na matakwa ya mwili.
Sio lazima mtu ufanye mazoezi magumu sana, kuna aina tofauti za mazoezi ambayo unaweza kuyatumia kwa afya. Kwa mfano kutembea umbali mrefu, kukimbia taratibu kwa umbali mrefu, kuendesha baiskeli na mazoezi ya viungo.
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Karolinska nchini Sweden, wamebainisha katika tafiti zao kwamba kutembea kwa kawaida kwa muda wa saa moja kwa siku, kwa muda wa siku tano kunaweza kushusha kiwango cha sukari kwa wagonjwa wa kisukari na kufikia kiwango cha kawaida kwa asilimia zaidi ya sabini.
Utafiti uliofanywa na wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba cha Muhimbili, hapa nchini umeonesha kwamba watu wenye tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara, wana kinga zaidi ya kutopata maradhi ya kisukari na moyo ukilinganisha na wale wasiofanya mazoezi kabisa.
Mbali na hayo, tafiti zimeonesha jamii zinazoishi vijijini na kujishughulisha na kilimo pamoja na ulaji wa vyakula vya asili ikiwemo kujishughulisha na shughuli zinazotumia nguvu, zimekuwa na kiasi kidogo sana cha magonjwa ya kisukari, moyo na saratani ikilinganishwa na jamii zinazoishi maisha tunayoyaita ya kisasa, ambapo watu hawapendi kabisa kusumbua miili yao.
Ikumbukwe kwamba mazoezi yanatambuliwa kama dawa katika nchi mbalimbali, mazoezi yana uwezo mkubwa wa kuzuia kisukari, ugonjwa wa moyo, unene wa kupindukia, saratani, magonjwa ya viungo, msongo wa mawazo na magonjwa ya mfumo wa homoni. Hakika kinga ni bora kuliko tiba, gharama ndogo itakayokugharimu kwa kufanya mazoezi, sio sawa na gharama kubwa itakayokukumba kwa kutibu magonjwa ambayo ungeweza kuyadhibiti kwa kufanya mazoezi tu.
Ni ngumu kuamini kwamba wakati mwingine unaweza kujiepusha na kifo kwa kufanya mazoezi, kwani watu wengi hupoteza maisha kwa kushambuliwa na magonjwa ambayo wangeweza kuyadhibiti na kuyaepuka kwa kufanya mazoezi, hapo unaweza kuona ni kwa kiasi gani mazoezi yalivyo muhimu katika maisha yako.
Baadhi ya watu wanadhani mazoezi ni kwa ajili ya kutengeneza maumbo mazuri ya miili tu, wengine wanaamini mazoezi ni kwa ajili ya watu wanene tu. Ukweli ni kwamba, mbali na kutengeza maumbo mazuri ya miili, lakini pia hata watu wasio na miili minene wanapaswa kufanya mazoezi kwani mazoezi, yanaboresha afya na kusaidia kuzuia magonjwa hatari mwilini.
Kwa wale wanaopenda kutumia lifti kuelekea katika ofisi zao, ni vyema wakatumia ngazi badala ya lifti au tumia lifti hadi ghorofa chache  kabla ya kufika katika ghorofa uendayo, kisha shuka kutoka katika lifti na umalizie kwa kupanda ngazi mbaka ufike unapoelekea.
Na kwa wale wanaotumia usafiri mara kwa mara, ni vyema ukatafuta sehemu ya umbali wa kiasi uliegesha gari lako, kisha tembea kwa miguu hadi ofisini kwako na endapo unafanya kazi zisizotumia nguvu, jitahidi kwa kiasi fulani kufanya kazi ukiwa umesimama, ili kuepuka kukaa kwa muda mrefu, ambapo itakusaidia kuepuka matatizo ya uti wa mgongo, na badala yake simama na tembeatembea hapo ofisini.
Wataalam wa masuala ya afya wanashauri kunywa maji ya kutosha baada ya kufanya mazoezi, kwa wale wanopenda kufanya mazoezi magumu kama vile kunyanyua vyuma vizito, inashauriwa kupata ushauri wa daktari kabla ya kuanza mazoezi hayo.
Nakushauri ndugu Mtanzania msomaji wa blog hii ya TABIBU, kama hujaanza mazoezi anza sasa na ukumbuke mwili wako ni kitu chenye thamani kubwa kuliko kitu kingine chochote hapa duniani.Hivyo basi, kuulinda mwili wako ni jukumu lako. Epuka kujibweteka na uanze kuupa mwili mazoezi ya kutosha ili kujenga afya bora. Kumbuka, mazoezi ni tiba.

Tiba asilia ya kisukari



Baada ya Alhamisi ya Julai 7 blog yako ya TABIBU kukuletea makala maalum iliyokuwa ikihusu ugonjwa wa kisukari, ambapo ulipata kufahamu aina za ugonjwa huo pamoja na visababishi vyake na dalili pia, sasa leo tunakuletea namna ambavyo tiba asilia inavyoweza kusaidia katika kutibu ugonjwa huo pamoja na mashuhuda waliozungumza na TABIBU Endelea sasa…. 
  
Mashuhuda waliopona kwa tiba asilia
Kupitia gazeti letu la TABIBU ambalo hupatikani mtaani kila siku ya Alhamisi lilifanikiwa kukutana na Tausi Miraji, ambaye ni mkazi wa Bagamoyo eneo la Mwanakalenge block P. Anasema mwaka 2009 alianza kujisikia mwili ukimuuma sana na alikuwa anakunywa maji mengi na kukojoa mara kwa mara, mwili ulikuwa na ganzi, mguu ulivimba na ulikuja kupasuka wenyewe tu, lakini alikuwa akibanwa na kiu.

Mara baada ya kuona dalili hizo anasema alilazimika kwenda kupima kisukari na aligundulika kweli alikuwa na kisukari, ambapo ilikua ni kiwango cha 33 na alipatiwa dawa, ingawaje anakiri kuwa dawa hizo zilikuwa zikimsaidia kutuliza maumivu. Lakini kwa muda wote huo, anasema alikuwa akiendelea kutafuta dawa za asili kwa ajili ya tatizo hilo ndipo siku mmoja mme wake alisoma gazeti hili na kusoma habari ya Dk. Mohamed Mkweli, ambaye aliainisha kutibu magonjwa mbalimbali hususani yale sugu.

 “Mme wangu siku moja alienda Dar es Salaam na kumtafuta daktari huyo na kisha aliniletea dawa za Dk. Mkweli na nikaanza kutumia, lakini ilinichukua miezi 6 kuanza kupata nafuu,ikiwa ni pamoja na kiu ya maji kukata, pamoja choo kidogo nilikuwa nikipata kama kawaida hata kusafiri safari ya mbali kwa sasa naweza,” alisema Bi Tausi.
 
Aidha, anaendelea kusema kuwa dawa hiyo ya daktari huyo ilikuwa ni ya rangi kama ya kijani ikiwa katika mfumo wa maji na inaitwa ‘Special 2.’ Lakini  pia, alipewa dawa ya kuchua ambayo anasema ilimsaidia sana kutuliza ganzi na  maumivu aliyokuwa nayo na hatimaye kiwango chake kilishuka hadi kufikia 5.

“Dawa za Mkweli mimi naamini zinasaidia, maana mimi nilitakiwa kukatwa mguu hospitalini kwa sababu ya kisukari, lakini nashukuru sana baada ya dawa za daktari huyo, kidonda changu kilipona na hadi sasa naendelea vizuri kabisa,” alisema Tausi.

Pamoja na hayo, aliongeza kuwa, “kwa sababu vidonge vya hospitalini unapomeza huwa  vinakwenda kunyamazisha tu na ikiamua kuanza  inaanza tena, Kwa sababu mimi wakati sijatumia dawa za Dk. Mkweli hii mifupa ilikuwa inaniuma vibaya sana, lakini ni vizuri watu wasiache kunywa dawa za hospitalini lakini wajaribu kutumia na dawa za asili pengine zinaweza kuwasaidia kama ilivyonisaidia mimi”.

Naye mme wa Bi Tausi, Bw. Kilagu Miraji anasema hata yeye hakuamini kama mguu wa mke wake ungepona na sukari ingeshuka na alikuwa anaamini kuwa mguu ungekatwa tu, lakini anasema baada ya dawa za asili kutoka kwa Dk. Mkweli, mguu huo ulipona na hata sasa madaktari wake wa hospitalini wanashangaa kuona mama huyo kapona kidonda hicho pamoja na sukari yake kushuka.

 Tiba asilia
TABIBU lilimtafuta Dk Mohamed Mkweli, anayemiliki kituo cha magonjwa sugu  kiitwacho Afya Bora, yeye anasema kweli Bi Tausi alikuwa ni mgonjwa wake na alianza kumtibu akiwa na kiwango cha sukari 33.

Nafarijika sana kusikia wagonjwa wanaotumia tiba zangu wanendelea vizuri na baadhi wamekuwa wakishuhudia kwa watu wengine. Kikubwa mimi napenda kuwasihi Watanzania kuendelea kuziamini tiba hizi za asilia zitokanazo na mimea, kwani ni nzuri na hazina kemikali kabisa na mfano mzuri ni dawa yangu hiyo ya ‘Special 2,’ ambayo imewasaidia wengi hadi sasa na jambo zuri zaidi dawa hii imepitishwa na mkemia mkuu, kwa hiyo si ya kubabaisha kabisa,” alisema Dk. Mkweli.

“Kwa mfano, kama Tausi, yeye  nilipoanza kumpatia dawa zangu kiwango chake cha sukari kilikuwa ni 33, lakini hivi baada ya kutumia hii ‘Special 2’ hivi karibuni amekwenda kupima ananiambia imeshuka hadi kufikia 5. Kwa hiyo utaona kuwa anaendelea vizuri na dawa imeonekana kumsaidia,” alisema Dk. Mkweli.

Hata hivyo, Dk. Mkweli anasema kuwa anashukuru kwa ushirikiano unaotolewa kwa Serikali kuhusu tiba asilia ingawaje anasema jitihada zaidi bado zinahitajika katika kuhakikisha tiba hizo zinakuwa ni mkombozi wa magonjwa sugu hapa nchini.

Sambamba na hayo, Dk. Mkweli anasema kwa sasa kupitia kituo chake hicho anaendesha kampeni ya kuangamiza magonjwa yote sugu yanayoaminika hayatibiki. Huku akiyataja baadhi ya magonjwa wanayotibu kwa sasa kuwa ni kisukari, shinikizo la damu (BP), matatizo ya figo, moyo mpana, kifafa, pumu na matatizo ya kina mama n.k. 

Dk. Mkweli anakiri kuwa changamoto kubwa waliyonayo kwa sasa ni katika kutibu UKIMWI na saratani ya muda mrefu ambayo bado wanatafutia tiba yake.

Hata hivyo, Dk. Mkweli anasema kwamba ana mpango wa kutoa ofa kwa viongozi wa Serikali ili na wao wajue tiba asili imefikia wapi na kwa kiasi gani inasaidia kutibu magonjwa sugu.

“Mimi baadaye nitatoa ofa kwa viongozi wa Serikali wa Tanzania bara na Zanzibar wenye tatizo la presha ili nao waje tuwatibu kwa gharama zetu ili waje wadhibitishe kuwa kweli tunatibu na wajue tumefikia wapi maana inawezekana. Hawajui tiba asili tumefikia 
 wapi,” alisema Dk. Mkweli.
 
Ni vyema ikafahamika kuwa mgonjwa wa kisukari anaweza kupata afueni kupitia vyakula, vidonge na insulini. Vyote hivi huweza kumsaidia mgonjwa kushusha kiwango cha sukari katika damu. Ingawaje matumizi ya vidonge na sindano husaidia kumtuliza mgonjwa na si kuponesha na pindi mgonjwa anapoacha kutilia mkazo katika matumizi ya tiba au kuacha kutumia dawa, ugonjwa hurudi tena. Hivyo ni vyema kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya muda wote.
Usikose gazeti lako la TABIBU kila Alhamisi mtaani ili uweze kufahamu habari nyingi pamoja na makala za afya kwa gharama ya shilingi 500/= tu.

Friday, August 8, 2014

Kumbe kisukari kinatibika na kuisha kabisa

  •  Daktari ajitokeza, asema anayo tiba asilia
  •    Ajinadi kutoa ofa kwa viongozi wa kitaifa kuwatibu bure
  • Mashuhuda waliopona wajitokeza 
Ugonjwa wa kisukari hujitokeza wakati ambapo kongosho hushindwa kuzalisha insulini ya kutosha au wakati mwili unaposhindwa kutumia insulini inayozalishwa kwa ufanisi. Insulini ni homoni inayosimamai kiwango cha sukari katika damu. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takwimu zinaonesha kuwa mnamo mwaka 2010 zaidi ya asilimia 80 ya vifo vya ugonjwa wa kisukari vimekuwa vikitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, huku wataalam wakisema kuwa, ifikapo mwaka 2030 idadi hiyo itaongezeka maradufu.

Sababu inayopelekea ugonjwa huu ni pamoja na mitindo ya maisha isiyofaa hususani maisha ya kisasa hasa kwa waishio maeneo ya mijini. Mitindo hiyo isiyofaa ni pamoja na aina ya vyakula vinavyoliwa, unywaji pombe na uvutaji sigara uliokithiri pamoja na kutofanya mazoezi ya mwili.

Inaelezwa kuwa mwaka 2004, watu  milioni 347 duniani kote walikuwa na kisukari, huku wastani wa watu milioni 3.4 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa wa huo.
Ugonjwa wa kisukari hutokea pale tezi kongosho (pancrease) inaposhindwa kutengeneza homoni au kichocheo aina ya insulini au mwili unaposhindwa kutumia vizuri kichocheo hicho cha insulini na kusababisha kuongezeka kwa kiwango cha sukari kwenye damu au kitaalam ‘hyperglycemia’.

Insulini ni kichocheo au homoni inayotengenezwa na kongosho ili kudhibiti sukari katika damu. Aidha, ugonjwa wa kisukari unaweza kusababisha kuwa na kiwango kidogo cha insulini mwilini au mwili kutosikia kichocheo hicho au yote mawili.

Ugonjwa huu huwaathiri watu wengi hata hapa nchini kwa sasa, huku wengi wakionekana kujigundua na ugonjwa huu mara tu wanapoanza kuona dalili  kuu  za kisukari, ambapo wengi huchelewa sana kugundua. (Look for Tanzania statistics)

Aina za kisukari
Aina ya kwanza ya kisukari (Type 1 - Diabetes Mellitus). Hii ni aina ya ambayo huwaathiri zaidi watoto na vijana. Aina hii hujitokeza pale ambapo seli maalum zinazotengeneza homoni ya insulin zinakuwa zimekosekana katika tezi kongosho au kuharibika kutokana na sababu yoyote ile, na hivyo kusababisha ukosefu kabisa au upungufu wa kichocheo hicho kwenye damu.

Mambo yanayoweza kusababisha uharibifu wa seli hizo katika tezi kongosho ni pamoja na kushambuliwa tezi kongosho kunakoweza kutokana na magonjwa ya kinga ya mwili ya mtu mwenyewe (autoimmune diseases) au kushambuliwa na vyanzo visivyojulikana.
Wagonjwa wa aina hii ya kisukari huhitaji kupewa dawa za insulini kwa njia ya sindano au pampu kila siku za maisha yao ili waweze kuishi. Kwa sababu hiyo,aina hii ya kisukari huitwa pia kisukari kinachotegemea insulini (Insulin Dependent Diabetes Mellitus) (IDDM). 

Aina nyingine ya kisukari ni kisukari aina ya pili (Type 2 - Diabetes Mellitus). Hii ni aina ya kisukari inayotokea zaidi ukubwani. Aina hii ya kisukari husababishwa na kupunguza utendaji kazi wa homoni ya insulin au seli kushindwa kutumia insulini ipasavyo. Hali hii mara nyingi husababishwa na unene uliopitiliza yaani ‘obesity,’ au hali ya kutoushughulisha kabisa mwili.

Katika aina hii ya kisukari, insulini huzalishwa kwa kiwango cha kutosha, isipokuwa tatizo hujitokeza katika suala la ufanisi na utendaji kazi wake na hii inamaanisha kwamba wagonjwa wa aina hii ya kisukari huwa hawahitaji kupewa insulin kwa njia ya sindano. Aina hii hujulikana pia kama kisukari kisichotegemea insulin (Non-Insulin Dependent Diabetes Mellitus).

Aidha, mbali na aina hizo mbili pia kuna aina ya tatu, ambayo ni kisukari cha mimba (Gestational Diabetes Mellitus). Aina hii hutokea pale kunapokuwa na ongezeko la kiwango cha sukari katika damu (hyperglycemia) wakati wa ujauzito.

Aina hii ya kisukari huathiri karibu asilimia 2 hadi 5 ya mama wajawazito wote, ingawa wengi wao hupata nafuu na kupona kabisa mara tu baada ya kujifungua. Hata hivyo, wajawazito ambao hupata aina hii ya kisukari huweza kuendelea kuwa na ugonjwa huo hata baada ya ujauzito na hatimaye kuwa na aina ya pili ya kisukari maishani.

Visababishi vya kisukari
·        Matumizi ya sukari nyingi na vyakula vya mafuta
·        Kurithi kutoka kwa wazazi
·        Unywaji wa pombe wa kupindukia
·        Kutofanya mazoezi
·        Anasa na starehe na mtindo wa maisha usiofaa
·        Kula vyakula vilivyotengenezwa kwa kuongezewa sukari, hasa vyakula vya viwandani (processed foods) n.k.
Dalili za kisukari
Kukojoa mara kwa mara, mgonjwa kuhisi kiu kali na kunywa maji kwa kiwango cha kupitiliza, mgonjwa kuhisi njaa na kula mara kwa mara, kuchoka haraka, mgonjwa kuwa na hasira, kupungua uwezo wa kufikiri pamoja na kusikia njaa n.k.

Mbali na dalili hizo, mgonjwa pia huweza kupata madhara ya muda mrefu, ambayo ni pamoja na kupata mtoto wa jicho na upofu, magonjwa ya figo, kupata magonjwa ya kinywa na kung’oka kwa meno, mwili kufa ganzi na kupoteza hisia hasa mikononi na miguuni, vidonda kutopona upesi na hatari ya kukatwa mguu.  Hata hivyo, madhara haya ya muda mrefu huweza kuzuilika endapo mgonjwa atafuata masharti ya wataalam wa afya hasa kuhusu chakula na mazoezi na maelekezo ya utumiaji sahihi wa dawa au insulini. 

Pia kuna hatari zaidi ya watu wanopatwa na kisukari kupatwa na magonjwa ya moyo, kiharusi, kuharibika kwa kibofu cha mkojo, shinikizo la juu la damu sambamba na ugonjwa wa fangasi.

Baada ya kufahamu hayo kuhusiana na ugonjwa huu wa kisukari, blog ya gazeti hili la tabibu jumamosi hii itakuletea mashuda waliopona pamoja na namna tiba asili inavyotibu na kumaliza kisukari. Hakikisha hukosi muendelezo wa makala hii.
Gazeti lako la TABIBU wiki hii lipo mitaani na unaweza kujipatia nakala yako kwa shilingi 500/= kila Alhamisi.

Thursday, August 7, 2014

Fahamu ubora wa mafuta ya samaki katika ubongo


Chicago, Marekani


Tafiti zinasema kuwa mafuta ya samaki aina ya Omega-3 yanaweza kusaidia ubongo kutokana na matatizo yanayosababishwa na pombe kwa asilimia 90.
Watafiti wamegundua kwamba seli za ubongo zilizohusishwa na kiasi kikubwa cha pombe ziliweza kulindwa zisiharibike na hatimaye kufa kwa mkusanyiko unaopatikana katika mafuta ya samaki.
“Mafuta ya samaki yana uwezo wa kusaidia kuutunza uwezo wa ubongo katika matumizi mabaya kabisa ya pombe,” alisema mtafiti Michael Collins kutoka Shule ya Madawa ya Chuo Kikuu cha Loyola, Chicago Marekani.
Katika utafiti huo, Collins na wenzake waliweka ubongo wa panya katika kiwango cha pombe kinachozidi mara nne ya kiwango kinachoruhusiwa kisheria kwa waendesha magari, kiasi cha pombe ambacho huwa kinaonekana kwa wanywaji pombe waliokubuhu.

NAMNA MIILI YETU INAVYOPOKEA SUMU


Karibu mpenzi msomaji wetu wa blog ya gazeti la TABIBU katika safu hii ya kutoka Miracle Food Clinic. Ambayo hupatikana ndani ya gazeti letu kila wiki Alhamisi, matumaini yangu u mzima wa afya tele.

Kuna vyakula vingi sana ambavyo vinaonekana kuvutia na kuwa na ladha nzuri mdomoni, lakini vita kubwa hufanyika wakati wa uyeyusho na katika ufanyaji kazi mwilini. Kwa mfano, mchanganyiko wa chumvi na kachumbari (salad) sio mzuri kiafya japokuwa una ladha nzuri, chumvi hufanya kazi ya kufyonza maji ambayo huondoka na virutubisho vyote unavyotegemea kuvipata kutoka kwenye kachumbari hiyo, hivyo kachumbari hubaki kuwa haina kazi mwilini.

Pia mpenzi msomaji unashauriwa kuepuka kuchanganya matunda machachu na matamu. Hii kwa ni sababu matunda machachu hupunguza kasi ya uyeyusho wa haraka wa sukari ya matunda matamu na kupelekea matunda matamu kuchacha.

Unaweza kujiuliza mbona vyakula hivi vinavyosemekana kuwa mchanganyiko wake ni hatari tumekuwa tukila kwa takribani maisha yetu yote bila athari? Jibu ni kwamba athari iletwayo na sumu ya vyakula, madawa, hewa na nyinginezo hutofautiana katika kutoa matokeo na kukujulisha kuwa unasumbuliwa na tatizo fulani. Hata hivyo, kumekuwa na magonjwa mengi makubwa yanayosumbua watu wengi huku wakijiuliza wamepata wapi athari hizo, kumbe ni mfumo uliojiwekea kwa kipindi kirefu na sasa ndio matokeo yake.

Tukiangalia mchanganyiko mwingine, tunakutana na kipengele cha vinywaji na vyakula vigumu,mfano chai, kahawa, pombe na vinywaji laini ukichanganya na chakula kigumu, mfano wa kitafunio, husababisha matatizo katika uyeyusho.
 
MSAMA KUWASHA MOTO WA HATARI KWA WEZI WA KAZI ZA WASANII, ZOEZI LIMEANZA RASMI

Kampuni ya Msama Promotions Ltd,kwa kushirikiana na Wizara ya habari vijana,utamaduni na michezo imetangaza neema kwa wasanii kuanza zoezi la kuwakamata watu wanaouza nakala feki za wasanii hapa nchini.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo,Bwana Alex Msama amesema hayo jijini dar ,kuwa zoezi hilo limekwishaanza, na mpaka sasa wamekamatwa vijana wane katika mkoa wa Dodoma na watatu jijini Mwanza.

‘’Kuna kazi mbalimbali ambazo zinaibiwa kila kukicha huku wamiliki wa kazi hizo wakiendelea kushuka kiuchumi na kutoona faida yoyote ya kazi hizo,huu ni wakati kwa wasanii kuneemeka na kazi zao.Hivyo tutahakikisha tunafika kila mahali hata sehemu zisizofikika kirahisi na yote hii ni kuonyesha kuwa tunajali na tunathamini kazi za wasanii wetu’’,alisema Msama kwa msisitizo.


Alisema, nakala zote zitakuwa na stika za TRA kuhakikisha hakuna wizi wowote unaofanyika na unaotokea katika kazi mbalimbali za wasanii.Stika hizo zimewekwa ili kuwabaini wale wote wenye hulka hiyo ya kuiba kazi za wasanii .Operesheni hiyo itafanyika bila kujali wadhifa wake ama cheo chake,akaongeza kusema kuwa zoezi hilo ni salamu kwa wale wote wanoatumia kazi za wasanii bila kufuata utaratibu wa sheria zilizopo.

Pia amelipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha katika changamoto,na pia wamekuwa wakishirikiana nao kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu na kuzunguka kila mkoa kuhakikisha kazi za wasanii zinaheshimiwa na zinalindwa kwa kila namna.

Inatoka kwa RUMAFRICA